Kiongozi wa kijeshi Mali achukua nafasi ya waziri wa ulinzi aliyeuawa
-
Assimi Goita
Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Assimi Goita, atachukua wadhifa mwingine wa Waziri wa Ulinzi, kwa mujibu wa dikrii iliyotangazwa kufuatia kuuawa waziri wa wizara hiyo katika mashambulizi makubwa ya hivi karibuni nchini humo.
Mali inakabiliwa na mgogoro wa usalama kufuatia mashambulizi dhidi ya ngome za kijeshi yaliyofanywa na kundi la Tuareg linalotaka kujitenga kwa kushirikiana na wanamgambo wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al -Qaida, ambapo Waziri wa Ulinzi Sadio Camara aliuawa kwa bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari katika makazi yake.
Wanamgambo wa Tuareg wanaotaka kujitenga huko Mali na wanamgamo wenye silaha wenye mfungamano na al Qaida walifanikiwa kuuteka mji muhimu wa kaskazini mwa Mali wa Kidal baada ya kushambulia maeneo na kambi nyingi za kijeshi nchini humo. Mashambulizi hayo yanatajwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kujiri Mali katika kipindi cha karibu miaka 15.
Watu wasiopungua 23 waliuawa katika mashambulizi hayo, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, likiripoti kuwa raia wa kawaida na watoto ni miongoni mwa waliouawa na kujeruhiwa katika hujuma hiyo.