YouTube yaifuta akaunti ya ‘Sovereign Media’ ya kupinga ubeberu nchini Kenya
-
YouTube imeiondoa njia ya Sovereign Media, chombo huru cha habari chenye makao yake Nairobi ambacho kinajulikana kwa msimamo wake wa kupinga ubeberu.
Kwa hatua iliyowashangaza wengi, YouTube imeiondoa bila taarifa ya awali akaunti ya Sovereign Media, chombo huru cha habari chenye makao yake Nairobi kinachojulikana kwa msimamo wake wa kupinga ubeberu.
Sovereign Media ni mshirika muhimu wa muungano wa vyombo vya habari vya kupinga ubeberu barani Afrika, muungano ulioanzishwa ili kuimarisha sauti kutoka majukwaa mbadala kama Black Agenda Report na Orinoco Tribune, vinavyoangazia migogoro ya kimataifa, harakati za muqawama, na maandamano dhidi ya vita kwa mtazamo wa kupinga ukoloni na unaounga mkono ujamaa.
Hatua hiyo ya kufuta chaneli hiyo ya YouTube ilitokea sambamba na siku ya ufunguzi wa mkutano wa “Forward Africa,” mkutano wa Afrika na Ufaransa uliofanyika Jumatatu na Jumanne jijini Nairobi wiki hii.
Sovereign Media iliripoti kuhusu maandamano dhidi ya ubeberu, yaliyofanyika Nairobi kupinga ziara ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron nchini Kenya.
YouTube – inayomilikiwa na shirika la Kimarekani la Google – imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji wa muda mrefu kutoka kwa wanahabari na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa kudhibiti, kufuta au kupunguza uwonekano wa maudhui yanayoonyesha misimamo ya kupinga ukandamizaji, kupinga ubeberu, na nyaraka za ukiukaji wa haki za binadamu.
Hatua ya kuifuta chaneli ya Sovereign Media imezua hasira na ukosoaji mpana.
Mtumiaji mmoja kwenye X ameandika. “Huu ni ukandamizaji wa kutisha. Pia, kama unataka kujua nini hasa kinautisha mfumo uliopo, na nini kina uwezo wa kukomesha ufisadi na unyanyasaji wa wenye mamlaka, angalia wanayemdhibiti, wanayemnyamazisha, na wanayemchafua."
Mtumiaji mwingine alisema kuwa huu ndio wakati Waafrika waanze “kuchukua hatua ya kujenga majukwaa yetu ya asili,” na kususia majukwaa makubwa kama YouTube.