Sheikh Zakzaky: Damu ya Imam Khamenei aliyeuawa shahidi itawaandama Wazayuni
-
Sheikh Ibrahim Zakzaky
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria amesema Imam Ali Khamenei aliyeuawa shahidi na damu yake safi vitaendelea kuuandama utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni sawa na donda la saratani.
Sheikh Ibrahim Zakzaky amesema hayo katika ujumbe wake kwenye sherehe ya uzinduzi wa tafsiri ya kitabu "Damu ya Moyo Iliyogeuka Kuwa Rubi" kwa lugha ya Kihausa kwamba: Imam Khamenei aliyeuawa shahidi na damu yake safi itauandama utawala wa Kizayuni.
Hafla ya uzinduzi wa tafsiri ya kitabu cha “Damu ya Moyo Iliyogeuka Kuwa Rubi” kwa lugha ya Kihausa ilifanyika Jumatatu, kwa ujumbe maalumu kutoka kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky katika mahfali iliyohudhuriwa na Dkt. Fatemeh Mohajerani, msemaji wa Serikali ya Iran, wasomi, wanaharakati wa masuala ya utamaduni na shakhsia mashuhuri wa vyuo vya kidini na kimataifa.
Kilele cha sherehe hiyo kilikuwa tangazo la ujumbe wa video kutoka kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria. Katika ujumbe wake, Sheikh Zakzaky amezungumzia historia ya familia na mapambano ya Imam Ali Khamenei na kumtaja kama mrithi mwadilifu wa Imam Khomeini (RA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu. Sheikh Zakzaky amesema kwamba kiongozi huyo aliyeuawa shahidi, licha ya majeraha aliyokuwa nayo kwa zaidi ya miongo minne, alikuwa akipiga hatua kwa azma thabiti na shauku ya ujana katika njia ya mapinduzi na kutetea Umma wa Kiislamu.
Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, Sheikh Zakzaky amemtaja Imam Khamenei kama shakhsia wa kipekee katika maarifa, ujasiri, fikra na uongozi, na kusisitiza kwamba wafuasi wa shahidi huyo wanaahidi kuendelea na njia yake.
Mwishoni mwa hotuba yake, kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria amezungumzia mustakabali wa kutia matumaini wa harakati ya haki dhidi ya ubeberu inayoongozwa na Imam Sayyid Mojtaba Khamenei akisema: Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Sayyid Mojtaba Khamenei, ataendeleza njia hii hadi ubeberu wa kimataifa utakapoangamizwa na kuanzishwa nguvu moja na kuu ya Mapinduzi ya Kiislamu.