Raia watano wa Msumbiji wauawa katika ‘Mashambulizi ya Chuki’ nchini Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138826-raia_watano_wa_msumbiji_wauawa_katika_mashambulizi_ya_chuki’_nchini_afrika_kusini
Serikali ya Msumbiji imetangaza kuwa takriban raia wake watano wameuawa katika “mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni” nchini Afrika Kusini mwishoni mwa juma lililopita. Vifo hivyo vinaashiria kushadidia maandamano yanayoendelea nchi nzima dhidi ya wahamiaji wasio na vibali.
(last modified 2026-06-02T09:06:01+00:00 )
Jun 02, 2026 09:01 UTC
  • Waandamanaji Afrika Kusini katika maandamano ya kupinga wahamiaji, Cape Town, Afrika Kusini, 23 Mei 2026.
    Waandamanaji Afrika Kusini katika maandamano ya kupinga wahamiaji, Cape Town, Afrika Kusini, 23 Mei 2026.

Serikali ya Msumbiji imetangaza kuwa takriban raia wake watano wameuawa katika “mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni” nchini Afrika Kusini mwishoni mwa juma lililopita. Vifo hivyo vinaashiria kushadidia maandamano yanayoendelea nchi nzima dhidi ya wahamiaji wasio na vibali.

Ofisi ya habari ya serikali ya Msumbiji, katika taarifa iliyopokelewa leo, imeeleza kuwa takriban Wamsumbiji 800 wameathiriwa katika ghasia zilizozuka kwenye mji wa pwani wa Mossel Bay, ulioko kusini mwa nchi hiyo, siku ya Ijumaa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa ghasia hizo ziliwalazimu Wamsumbiji 300 kurejea nyumbani siku ya Jumamosi. “Wengine waliosalia, zaidi ya 500, wamehifadhiwa katika eneo salama katika Jimbo la Rasi ya Magharibi (Western Cape), na kufikia leo, Juni 1, mchakato wa kuwarejesha nchini Msumbiji ukiwa tayari umeanza.”

Ukanda huo umeshuhudia maandamano dhidi ya wahamiaji yanayofanana na yale yaliyoripotiwa katika kitovu cha kifedha cha Johannesburg, mji wa Durban, na sehemu za Jimbo la Rasi ya Mashariki (Eastern Cape) katika wiki za hivi karibuni.

Afrika Kusini imekuwa ikikabiliwa na mawimbi ya mara kwa mara ya ghasia za chuki dhidi ya wageni tangu mwaka 2008, ambapo makumi ya wahamiaji waliuawa na maelfu kuyahama makazi yao katika mashambulizi yaliyotokea nchi nzima. Machafuko kama hayo yalijirudia tena mwaka 2015 na 2021.

Ongezeko hili la sasa la mvutano dhidi ya wahamiaji linakuja wakati vyama vya kisiasa nchini humo vikitafuta uungaji mkono kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba.