Sep 01, 2016 03:41 UTC
  • Uchumi wa taifa la Nigeria waporomoka

Takwimu zilizotolewa kuhusu pato la ndani la taifa zinaonyesha kuwa, uchumi wa nchi ya Kiafrika ya Nigeria umeporomoka. Takwimu hizo zinaonesha kuwa, uchumi wa taifa hilo lenye uchumi mkubwa barani Afrika ulishuka kwa zaidi ya asilimia 2% katika robo ya pili ya mwaka huu.

Habari kutoka Nigeria zinasema kuwa, hasara hii ya kiuchumi si jambo lililowashtua mamilioni ya raia wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Raia wengi wa nchi hiyo wanasema kuwa, hawajawahi kushuhudia ugumu wa maisha kama walio nao sasa. Kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kunatajwa kuwa moja ya sababu kuu zilizoathiri vibaya uchumi wa Nigeria. 

Serikali ya Nigeria inaegemea mauzo ya mafuta kwa takriban asimilia 70% ya mapato yake. Lakini wakosoaji wanasema sera za serikali zimeifanya hali kuwa mbaya zaidi. Hivi sasa ughali wa maisha unashuhuhudiwa katika akthari ya miji ya nchi hiyo na kuna uwezekano hali ikawa mbaya zaidi katika miezi ijayo.

Rais Buhari wa Nigeria

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanailalamikia serikali ya sasa ya Nigeria kutokana na kushughulishwa mno na vita dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram na kusahahu masuala mengine. 

Zaidi ya watu 30,000 wameuawa hadi sasa nchini humo kutokana na mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, mbali na mamia ya nyumba na maeneo ya vijiji kuchomwa moto na kundi hilo.

Katika miaka ya karibuni, mashambulio ya kundi la Boko Haram ambalo ngome yake kuu iko katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria yamezilenga pia nchi jirani za Chad, Cameroon na Niger.

Tags