Mivutano ya kisiasa yaongezeka kati ya Sudan na Sudan Kusini
Duru za nchini Sudan zimekosoa upuuzaji unaofanywa na Sudan Kusini katika kuwadhibiti waasi waliopo katika maeneo ya mipaka ya nchi mbili hizo.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ambaye hakutajwa jina lake litajwe ametishia kuwa Sudan Kusini inapasa kuchukua hatua za lazima na kuyafukuza makundi ya uasi yaliyoko katika maeneo ya mpakani ya nchi hiyo. Afisa huyo wa Sudan amesema kuwa nchi hiyo itafunga mipaka yake na jirani yake Sudan Kusini iwapo haitatekeleza ahadi yake ya kuyafukuza makundi ya uasi yanayopigana na Khartoum.
Hii ni katika hali ambayo Taban Deng Makamu wa Rais wa Sudan Kusini wiki kadhaa zilizopita alifanya safari huko Khartoum mji mkuu wa Sudan kwa ajili ya mashauriano ya kisiasa na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo; ambapo ajenda kuu ya mazungumzo yao ya kisiasa ilikuwa ni kuipatia ufumbuzi mivutano ya kisiasa kati ya nchi mbili hizo.
Baada ya mazungumzo hayo Deng aliwahakikishia viongozi wa Khartoum kuwa waasi walipo katika maeneo ya mpakani watafurushwa huko Sudan Kusini katika muda wa siku 21. Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Kusini pia siku kadhaa zilizopita ilisisitiza kuhusu kupatiwa haraka iwezekakanavyo ufumbuzi mivutano ya kisiasa iliyopo.