Wahamiaji 29 wafariki dunia nchini Misri baada ya boti kuzama
Boti iliyokuwa imebeba wahamiaji haramu wapatao 600 imezama katika pwani ya Misri na kupelekea kwa uchache watu 29 kufariki dunia.
Ripoti zinasema kuwa, boti hiyo ilikuwa imewabeba abiria 600,ambao kati yao 150 wameokolewa kulingana na chombo cha habari cha taifa hilo.
Kwa mujibu wa duru za Misri hadi jana Jumatano miili ya wahanga 29 wa ajali hiyo ilikuwa imepatikana ambapo 18 ni wanaume, 10 ni wanawake na mtoto mmoja mdogo.
Taarifa za awali zinasema kuwa, boti hiyo ilizama kutokana na kupakia abiria kupita kiasi. Wahamiaji hao waliokuwa wakielekea Ulaya ni raia wa Misri, Syria na baadhi ya nchi nyingine za Kiafrika.
Takwimu mpya za Shirika la Wahajiri Duniani zinaonyeshah kuwa tangu kuanza mwaka huu wa 2016 hadi sasa, wahajiri karibu laki moja na elfu tano; ambao wengi walitokea Libya walifanikiwa kuingia nchini Italia. Katika kipndi hicho wanaume, wanawake na watoto 2,726 pia walizama majini kabla ya kufika katika nchi waliyokuwa wakielekea.
Aidha kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, tangu mwaka 2014 hadi sasa zaidi ya wahajiri elfu 10 waliokuwa wanaelekea Ulaya kupitia njia ya bahari, wamepoteza maisha.
Wahamiaji hao haramu wengi wao wamekuwa wakitokea katika nchi za Libya, Misri, Algeria, Morocco, Somalia, Sudan na Ethiopia.