Magaidi 12 wauawa Sinai Kaskazini nchini Misri
Duru moja ya kijeshi ya Misri imetangaza habari ya kuuawa magaidi 12 katika mapigano yaliyozuka Sinai Kaskazini kati ya jeshi la nchi hiyo na magaidi hao.
Televisheni ya Sky News imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, magaidi hao 12 wameuliwa na jeshi la Misri katika eneo la Hayyu al Tarabin na kwenye kijiji cha al Dhahir katika eneo la Sheikh Zuweid, kaskazini mwa Rasi ya Sinai huko Misri.
Habari nyingine zinasema kuwa, maafisa wa kulinda usalama wa Misri, jana walivamia mji wa al Arish na kuwatia mbaroni watu 200 kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya kigaidi.
Ni vyema kusema hapa kuwa, kundi la kigaidi linalojiita Ansar Bait al Muqaddas, ni kundi hatari mno la kigaidi katika eneo la Sinai Kaskazini nchini Misri. Kundi hilo linajiita Wilaya ya Sinai na limetangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la Daesh.
Kwa upande wake, jeshi la Misri limekuwa likifanya opereseheni mbalimbali kubwa na ndogo katika eneo hilo kwa muda mrefu sasa kwa ajili ya kukabiliana na magaidi hao ambao wamehusika katika mashambulizi mengi ya kigaidi kwenye maeneo tofauti ya Misri.