Oct 07, 2016 07:57 UTC
  • Waislamu Nigeria walionya jeshi la nchi hiyo

Kiongozi mwandamizi wa harakati ya Kiislamu nchini Nigeria amelionya jeshi la nchi hiyo kutokana na vitendo vyake vya kikatili na visivyo vya kibinaadamu dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.

Bashiru Marta, amesema kuwa, ukatili wa jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu na kadhalika kitendo cha serikali ya nchi hiyo cha kutozingatia matakwa yao ya kumuachilia huru Sheikh Ibrahim Yaqoub El Zakzaky, ni mambo yanayoshadidisha hasira za Waislamu nchini humo. Amesisitiza kuwa, takwa kuu la Waislamu wa Nigeria ni kuachiliwa huru haraka iwezekanavyo sheikh huyo na bila ya masharti yoyote.

Sehemu ndogo ya jinai zilizofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu wa Shia nchini humo

Hii ni katika hali ambayo Waislamu nchini humo wamekadhibisha madai ya hivi karibuni ya jeshi la serikali lilipodai kwamba harakati hiyo ina lengo la kuchochea machafuko. Wamesisitiza kuwa, kwa kipindi cha miongo kadhaa ya tangu kuanzishwa harakati hiyo nchini Nigeria, wanachama wake wamekuwa wakijishughulisha tu na shughuli za kijamii na kisiasa kwa mujibu wa sheria kama ambavyo hawajawahi kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.

Kadhalika wameipa serikali ya Abuja muhula wa wiki moja tu kuhakikisha inamuachilia huru Sheikh Ibrahim Yaqoub El Zakzaky na mke wake na kwamba kinyume na hivyo serikali hiyo itabeba dhima ya machafuko yatakayotokea nchini humo. 

Tags