Oct 12, 2016 07:35 UTC
  • Mkutano kuhusu haki za wanawake waanza Tanzania

Wanawake kutoka nchi kadhaa za Afrika wanakongamana mjini Moshi nchini Tanzania katika mkutano wa kujadili haki za mwanamke, hususan haki ya kumiliki ardhi na maliasili.

Mkutano huo wa siku tatu unaanza leo kwa washiriki hao kukwea Mlima Kilimajaro, kuashiria machungu na changamoto wanazopitia wanawake kila uchao, haswa ikija katika suala la kutaka kumiliki ardhi.

kwa mujibu wa James Butare, Mkuu wa Mipango na Sera wa shirika la Action Aid ambalo ni moja ya taasisi zinazofadhili kongamano hilo, akthari ya wanawake wanaoshiriki mkutano huo uliopewa jina la "Kilimanjaro Initiative" wanatoka katika maeneo ya vijijini katika nchi 20 za bara Afrika.

Kwa muda mrefu, wanaume ndio wamekuwa wakimiliki vipande vya ardhi na mashamba barani Afrika

Amesema miongoni mwa vizingiti vinavyowafanya wanawake washindwe kumiliki ardhi ni ndoa za mapema, ukosefu wa taarifa muhimu na tamaduni zilizopitwa na wakati zinazomnyima mwanamke haki ya kurithi au kumiliki ardhi.

Katika hali ambayo Umoja wa Afrika ulitangaza mwaka huu 2016 kuwa mwaka wa kutetea haki za binadamu hususan za wanawake, takwimu za hivi karibu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO zinaonyesha kuwa, asilimia 25 ya vipande vya ardhi vinavyotumika kwa kilimo katika nchi zilizostawi kiuchumi vinamilikiwa na wanawake, kinyume kabisa na taswira inayoshuhudiwa katika nchi zinazokuwa barani Afrika.

Tags