Wanafunzi elfu 80 kuacha shule kutokana na njaa Zimbabwe
(last modified Wed, 19 Oct 2016 15:28:14 GMT )
Oct 19, 2016 15:28 UTC
  • Wanafunzi elfu 80 kuacha shule kutokana na njaa Zimbabwe

Wanafunzi zaidi ya 80,000 nchini Zimbabwe wapo katika hatari ya kukatiza masomo yao kutokana na baa la njaa ambalo limefikia "kiwango cha kutisha."

Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), mikoa iliyoathiriwa zaidi na ukame na baa la njaa nchini humo ni Matebeleland Kaskazini, Midlands na Mashonaland ya Kati.

Wanafunzi wengi Zimbabwe wanategemea mlo wa shule

Shirika la WFP limetangaza kuwa, linahitajia kiasi cha dola milioni 290 za Marekani kwa ajili ya kutoa misaada ya kibinadamu kwa wananchi milioni 4.5 wa Zimbabwe kufikia mwishoni mwa mwaka ujao.

Mapema mwaka huu Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alitangaza ukame ulioikumba nchi hiyo kuwa ni janga la kitaifa.

Hivi karibuni serikali ya Harare iliomba msaada wa dola bilioni moja na milioni 600 kwa ajili ya kununua nafaka na bidhaa nyengine za chakula.

Maandamano ya wanachi dhidi ya serikali ya Zimbabwe

Katika wiki za hivi karibuni, Zimbabwe imeshuhudia maandamano ya wapinzani wanaomtaka Rais Mugabe aondoke madarakani wakisisitiza kuwa, ameshindwa kutatua matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa ajira nchini humo.