Ufaransa yasisitiza udharura wa kuendelea kuwepo jeshi la nchi hiyo huko Mali
Waziri Mkuu wa Ufaransa amesisitiza ulazima wa kuendelea kuwepo wanajeshi wa nchi hiyo huko Mali.
Manuel Valls ametangaza katika bunge la Ufaransa kuwa njia ya kupatikana utulivu na amani ya kudumu nchini Mali ni ndefu sana. Kiongozi huyo wa Ufaransa amesema, kwa kuzingatia vitisho vitisho vinavyoendelea kutolewa na magaidi huko Mali na kuchelewa mchakato wa kupatikana suluhu ya kitaifa nchini humo, upo udharura wa kuendelea kuwepo wanajeshi wa Ufaransa nchini Mali.
Waziri Mkuu wa Ufaransa ameongeza kuwa, kuna hatari ya makundi ya kigaidi kudumisha machafuko na hali ya mchafukoge katika eneo la Sahel barani Afrika na kupanga mashambulizi makubwa zaidi.
Emanuel Valls amewataka wanajeshi wa nchi yake waendelee kuwepo Mali katika hali ambayo ni miaka kadhaa sasa wanajeshi wa Ufaransa wako katika nchi hiyo ya Kiafrika kwa kisingizio cha kusaidia kurejesha amani nchini humo. Siku kadhaa zilizopita Rais Francois Hollande wa Ufaransa alifanya mazungumzo na Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali ambapo alisisitiza azma ya nchi yake ya kutaka kushirikiana na serikali ya Mali ili kufanikisha utelekezaji wa makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwaka 2015. Rais wa Ufaransa alieleza kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo wamejiandaa kushiriki katika doria katika maeneo ya kaskazini mwa Mali kwa kushirikiana na jeshi la nchi hiyo na makundi yaliyosaini makubaliano ya amani ya Algeria.
Hali ya machafuko na ukosefu wa amani imekuwa ikiisumbua nchi ya Mali kwa miaka kadhaa sasa. Kundi la wanamgambo wa Tuareg na wapinzani wa serikali wanaendelea kukabiliana na serikali kuu licha ya kusainiwa makubaliano ya amani; na mashambulizi yanayofanywa na makundi hayo yanavuruga utulivu wa maeneo mbalimbali hususan eneo la kaskazini mwa Mali.
Kwa muda sasa serikali ya Paris imekuwa ikitilia mkazo suala la kuendelea kuwepo wanajeshi wake nchini Mali katika kile inachokitaja kuwa ni kusaidia juhudi za kurejesha amani na utulivu nchini humo. Hata hivyo baadhi ya weledi wa mambo wanakumbusha nafasi ya Ufaransa na baadhi ya nchi za Magharibi katika machafuko ya sasa huko kaskazini mwa Mali. Weledi hao wanasema Ufaransa imekuwepo siku zote katika nchi nyingi za Kiafrika zikiwemo zile za Sahel na kuzitumia nchi hiyo kufanikisha maslahi yake ya kikoloni kwa kutekeleza siasa zake za kuingilia kati na za nyuma ya pazia kwa kutumia kisingizio cha kusaidia kurejesha amani katika nchi hizo.
Ukame na uhaba wa chakula, harakati za magenge ya mihadarati na magendo ya binadamu, kuongezeka wahamiaji haramu, makundi yenye misimamo mikali na vitendo vya kigaidi, ni masuala ambayo yamekuwa hatari kubwa kwa nchi nyingi za eneo hilo.
Matatizo hayo yote pamoja na ufisadi wa kiuchumi, watawala madikteta na kutoheshimiwa sheria na misingi ya demokrasia, kwa mara nyingine tena kumezipatia kisingizio baadhi ya nchi za Magharibi hususan Ufaransa kupora maliasili na utajiri wa nchi nyingi hususan za Kiafrika kupitia njia ya kutuma vikosi vya majeshi yao kwenye nchi hizo kutekelezwa siasa zao za kibeberu.
Kwa msingi huo viongozi wa nchi mbalimbali za eneo la Sahel huko Afrika wanapasa kuweka kando hitilafu za kikabila, kikaumu na kidini na badala yake waunganishe pamoja nguvu zao za ndani na za kieneo ili kuboresha hali za nchi hizo na kuendesha vita dhidi ya makundi yenye misimamo mikali; na hivyo kuziba myanya unayotumwia na nchi za kigeni kwa ajili ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi hizo.