Wawili wahukumiwa kunyongwa nchini Misri kwa ugaidi
-
Askari wa Misri wakiwa katika ulinzi mkali
Mahakama moja nchini Misri imewahukumu kifo watu wawili kwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi na wengine 12 vifungo virefu na vifupi kwa kosa hilo hilo.
Shirika la habari la IRIB limevinukuu vyombo vya mahakama vya Misri vikitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, mahakama ya rufaa ya Cairo imetoa hukumu hiyo leo Jumamosi.
Mahakama hiyo aidha imesema, watu hao wamepatikana na hatia ya kufanya njama za kushambulia maeneo ya serikali, kumiliki silaha na kuunda makundi kinyume cha sheria.
Taarifa zinasema kuwa watu hao walijiunga na magenge yenye misimamo mikali nchini Libya na walitiwa mbaroni wakati walipokuwa njiani kurejea nchini Misri.
Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Misri wana wasiwasi wa kutokea machafuko na mashambulizi ya kutumia silaha kutoka kwa watu ambao wamewahi kutembelea Libya na kujiunga na magenge ya kigaidi kama vile Daesh.
Ikumbukwe kuwa, tangu miaka miwili nyuma hadi hivi sasa, watu wenye silaha wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kuvizia dhidi ya viongozi na maafisa wa kulinda usalama pamoja na vituo vya kijeshi na vya polisi katika maeneo tofauti ya Misri hususan kwenye mkoa wa Sinai Kaskazini na wameshaua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.