Mahakama ya Jinai Misri yawahukumu watu 47 vifungo tofauti
Mahakama ya Jinai nchini Misri imetoa hukumu ya vifungo vya miaka 7 hadi 15 jela kwa watu 47 baada ya kuwapata na hatia ya kupiga kambi katika Medani ya Rābiʻa al-ʻAdawiyya nchini humo.
Mahakama ya mjini Cairo imewahukumu watu 21 kifungo cha miaka 15 jela, watu 15 kifungo cha miaka 10 jela na watu 11 wengine kifungo cha miaka saba jela. Mahakama hiyo imedai kuwa watu hao walihusika katika machafuko, vitendo vya ukatili na kutumia silaha kuvuruga usalama na kupelekea raia kadhaa na polisi kuuawa.
Wiki iliyopita pia, mahakama ya Misri ilisikiliza kesi ya Mohammed Badie, kiongozi wa kundi la Ikhwanul Muslimin na kadhalika wafuasi 783 wa kundi hilo lililopigwa marufuku na serikali ya hivi sasa ya nchi hiyo kwa tuhuma za kushiriki katika maandamano na kupiga kambi katika Medani ya Rābiʻa al-ʻAdawiyya .
Hata hivyo kesi hiyo iliakhirishwa hadi tarehe 19 ya mwezi huu. Itakumbukwa kuwa, mwezi Agosti mwaka 2013 polisi ya Misri iliwashambulia wafuasi wa rais wa zamani wa nchi hiyo Muhammad Mursi katika Medani za Rābiʻa al-ʻAdawiyya na al-Nahdha ambapo mamia ya waandamanaji waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.