Mahakama ya rufaa Misri yafuta adhabu ya kifo dhidi ya Muhammad Mursi
Mahakama ya rufaa nchini Misri, sanjari na kukubali malalamiko ya Muhammad Mursi, rais wa zamani aliyeondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi, imefuta adhabu ya kifo iliyokuwa imetokewa dhidi yake.
Mahakama hiyo ya rufaa imechukua uamuzi huo katika kikao cha dakika chache kilichofanyika Jumanne ya jana ambapo mbali na kukubali malalamiko ya rais huyo wa zamani na baadhi ya viongozi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin, imewafutia pia adhabu ya kifo na kifungo cha maisha, huku faili la kesi hiyo likitumwa mahakama nyingine kwa ajili ya kuchunguzwa upya.
Itakumbukwa kuwa Januari mwaka jana 2015, mahakama ya jinai ya Misri, ilimuhukumu adhabu ya kifo Muhammar Mursi na baadhi ya viongozi wa harakati hiyo iliyopigwa marufuku katika faili lililopewa jina la 'Shambulio dhidi ya Wafungwa.' Mahakama hiyo iliwahukumu pia kifungo cha maisha viongozi wengine 21 wa Ikhwanul Muslimin, sambamba na kuwahukumu kifungo cha miaka miwili jela makamanda wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon.
Kabla ya hapo, mahakama ya rufaa nchini Misri, ambayo ni mahakama ya juu ya kiraia nchini Misri ilitoa adhabu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya rais huyo wa zamani wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika kuhusu faili la kufanya ujasusi kwa maslahi ya Harakati ya Kiislamu ya muqawama ya HAMAS na serikali ya Qatar.