Mtandao mkuu wa kuuza viungo vya wanadamu Misri wavunjwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i20935-mtandao_mkuu_wa_kuuza_viungo_vya_wanadamu_misri_wavunjwa
Misri imevunja mtandao mkubwa ambao umekuwa ukifanya magendo ya viungo vya wanadamu katika nchi mbali mbali duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 07, 2016 04:18 UTC
  • Mtandao mkuu wa kuuza viungo vya wanadamu Misri wavunjwa

Misri imevunja mtandao mkubwa ambao umekuwa ukifanya magendo ya viungo vya wanadamu katika nchi mbali mbali duniani.

Hayo yamefichuliwa na Wizara ya Afya ya nchi hiyo na kubainisha kuwa, watu 45 wanaohusishwa na mtandao huo wamekamatwa, wakiwemo madaktari, wauguzi, mawakala na wanunuzi wa viungo hivyo.

Habari zaidi zinasema kuwa, miongoni mwa madaktari waliokamatwa wamekuwa wakihudumu katika taasisi mashuhuri za afya nchini humo na wengine ni wahadhiri katika vyuo vikuu vya Cairo na Ainu Shams, taasisi mbili kuu za masomo ya juu nchini humo. Aidha mamilioni ya dola za Marekani zimepatikana katika vituo vya afya vya kibinafsi ambapo biashara hiyo haramu imekuwa ikifanyika. Baadhi ya hospitali na zahanati hizo zimesajiliwa na serikali ijapokuwa aghalabu yake hazijaidhinishwa na Wizara ya Afya.

Wahajiri wanaoelekea Ulaya, wahanga wakuu wa magendo ya viungo

Ingawaje magendo ya viungo vya wanadamu ni kinyume cha sheria nchini Misri, lakini umasikini na uchochole umewasukuma Wamisri wengi kuingia katika mtego wa mtandao huo haramu.

Inaarifiwa kuwa, wanaofanya magendo ya viungo vya watu nchini humo wamekuwa wakiwalenga wahamiaji wanaotaka kwenda bara Ulaya kupitia safari hatari za baharini na wasiokuwa na pesa za kukidhi haja zao.

Sio vibaya kukumbusha hapa kuwa, mwezi Machi mwaka huu, taasisi moja ya kuwahami watoto wa Kiafrika ilitangaza kuwa, katika uchaguzi wa Februari nchini Uganda, watoto sita waliuawa au kukatwa viungo vyao vya mwili kutokana na imani za kishirikina.