Watoto 17,000 watumika kama askari Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i21589-watoto_17_000_watumika_kama_askari_sudan_kusini
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limesema kuna watoto elfu 17 wanaotumiwa kama askari wa makundi ya wapinzani nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 17, 2016 04:31 UTC
  • Watoto 17,000 watumika kama askari Sudan Kusini

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limesema kuna watoto elfu 17 wanaotumiwa kama askari wa makundi ya wapinzani nchini Sudan Kusini.

Taarifa ya UNICEF inasema tangu mapigano yalipoibuka baina ya wapiganaji wa waasi na jeshi la serikali miaka mitatu iliyopita nchini Sudan Kusini watoto elfu 17 wameingizwa katika makundi ya waasi kutumika kama askari.

Takwimu zilizotolewa na shirika hilo zimeonyesha kuwa, mpaka sasa ni askari watoto 1,932 tu wameachiwa huru.

Kuanzia mwaka huu, Shirika hilo na mashirika mengine yamepokea watoto laki 1.8 wanaokabiliwa na utapiamlo, na idadi hii imeongezeka kwa asilimia 50 kuliko mwaka jana.

Salva Kiir (kushoto) na Riek Machar

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa pia imesema serikali imekuwa ikiwatumia watoto kama askari jeshini na kuongeza kuwa tokea mwaka 2013,watoto 2,342 wameuawa au kujeruhiwa vitani Sudan Kusini huku wengine 3,090 wakitekwa nyara, na 1,130 wakidhalilishwa kijinsia.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.