Wamisri waingiwa na wasiwasi wa kuvamiwa nchi yao na wimbi la magaidi
-
Magaidi wa ISIS katika rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri wakijiandaa kuwapiga risasi mateka.
Duru za usalama nchini Misri zimetangaza habari ya uwezekano wa kuvamiwa nchi hiyo na wimbi la magaidi kutoka nchi nyingine, suala ambalo limezitia hofu nyoyo za wananchi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Shirika la habari la Sky News limezinukuu duru za usalama za Misri zikisema kuwa, baada ya magaidi kupata pigo kubwa katika mashambulizi ya kupambana na magaidi huko Syria, Iraq na Libya, magaidi hao wameamua kurejea katika nchi zao na wengine kutafuta maficho kwenye nchi nyinginezo ikiwemo Misri.
Kwa mujibu wa ripoti hiyio, duru za usalama za Misri zimetangaza habari ya kutiwa mbaroni kundi moja la magaidi wenye uhusiano na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) katika siku za hivi karibuni.
Duru rasmi za usalama za Misri zimesema kuwa, nchi hiyo imeamua kuchukua hatua za ziada za kiusalama kukabiliana na wimbi la kuingia nchini humo makundi ya kigaidi kupitia mipaka ya nchi hiyo.
Hivi karibuni pia, maafisa usalama wa nchi jirani ya Tunisia waliwatahadharisha viongozi na wananchi wa nchi hiyo na kuwataka wachukue hatua za ziada za kukabiliana na misimamo mikali ili kuzuia vijana wa nchi hiyo kujiunga na makundi ya kigaidi ya nje ya Tunisia baada ya kuongezeka uwezekano wa kurejea Tunisia magaidi waliopata pigo katika nchi za Syria, Iraq na Libya.
Ikumbukwe kuwa, hali ya kiusalama, kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo imepelekea mamia ya raia wa Tunisia kujiunga na magenge ya kigaidi na matokeo yake ni kuhatarisha usalama na amani ya nchi hiyo wakati wanaporejea nchini humo.
Hivi karibuni pia mamia ya watu walikusanyika mbele ya Bunge la Tunisia kulalamikia ruhusa ya kurejea nchini humo, watu wenye misimamo mikali. Kwa mujibu wa sheria iliyopasishwa mwaka 2015 na Bunge la Tunisia, watu waliojiunga na magenge ya kigaidi nje ya Tunisia, wana haki ya kurejea nchini humo kama raia.