Msalaba Mwekundu: Wakenya milioni 2.4 katika hatari ya kufa njaa
(last modified Sat, 07 Jan 2017 07:38:39 GMT )
Jan 07, 2017 07:38 UTC
  • Msalaba Mwekundu: Wakenya milioni 2.4 katika hatari ya kufa njaa

Shirika la Msalaba Mwekundu limeonya kuwa, mamilioni ya Wakenya wapo katika hatari ya kukumbana na baa la njaa katika miezi michache ijayo.

Leila Chepkemboi, Mkurugenzi wa Mipango Maalumu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya amesema kuwa, watu milioni 2.4 katika nchi hiyo ya Afrika watakabiliwa na njaa kali kutokana na ubaha wa chakula kufikia mwezi Aprili mwaka huu.

Chepkemboi ameliambia gazetil la The Star linalochapishwa nchini humo kuwa, dalili zote zinaashiria kuwa kaunti nane zitashuhudia uhaba mkubwa wa chakula mwezi Aprili.

Sehemu ya athari za ukame nchini Kenya

Amezitaja kaunti hizo kuwa ni pamoja na Kwale, Mandera, Marsabit, Samburu na Garissa. Kaunti zingine zitakazoshuhudia baa la njaa miezi michache ijayo ni Kilifi, Lamu na Tana River.

Mkurugenzi wa Mipango Maalumu ya Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya ameongeza kuwa, maeneo ya Laikipia, Kitui, Turkana, Marakwet na Pokot yamekuwa yakishuhudia migogoro na mapigano kutokana na ukame uliopelekea maelfu ya mifugo kufa.

Mapema mwezi huu Umoja wa Mataifa ulisema kuwa una wasiwasi kuhusu maafa yanayosababishwa na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ya El-Nino katika maeneo ya kaskazini na mashariki mwa Afrika.