Watu 12 wafariki dunia kwa kuzama maji nchini Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23245-watu_12_wafariki_dunia_kwa_kuzama_maji_nchini_tanzania
Watu 12 wameripotiwa kufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama baharini nchini Tanzania.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 11, 2017 01:20 UTC
  • Watu 12 wafariki dunia kwa kuzama maji nchini Tanzania

Watu 12 wameripotiwa kufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama baharini nchini Tanzania.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, mashariki mwa Tanzania amenukuliwa akisema kuwa boti hiyo iliondoka siku tatu zilizopita kutoka pwani ya mkoa huo kuelekea Wete, Pemba Zanzibar. Kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi, watu hao wamefariki dunia baada ya boti hiyo kupinduka baharini na kwamba miongoni mwa wahanga wa ajali hiyo ni pamoja na wanaume watano na wanawake saba.

Baadhi ya watu walionusurika katika ajali wakibebwa na polisi

Hii ni katika hali ambayo baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kwamba miili ya watu 13 iliokotwa Jumanne ya jana akiwemo nahodha ya boti hiyo. Habari zaidi zinasema kuwa, ajali hiyo ilitokea eneo la Gambe Pemba, na kwamba wengi wa wasafiri wa boti hiyo walikuwa ni wanafunzi waliokuwa wakirudi shuleni baada ya likizo ya mwezi Disemba kumalizika. Baadhi ya watu walionusurika katika ajali hiyo wamesema kuwa, boti hiyo ilikumbwa na upepo mkali na kupasuka vipandevipande na kwamba, walikuwemno abiria zaidi ya 50, huku wengine wakiwa hawajulikani walipo. “Baada ya kuondoka bandarini nahodha pamoja na wasaidizi wake walilazimika kusimamisha chombo kwa takribani saa mbili hivi ili kupisha upepo na baadaye tukaondoka, lakini hatukufika mbali chombo kikapigwa na wimbi na kupoteza mwelekeo ambapo baadaye kilijaa maji na kukatika katikati," anasimulia Emmanuel Mniga, mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, mkazi wa mkoa wa Morogoro, ambaye amelazwa katika wodi ya A1 katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo, Tanga.

Wahanga wa baadhi ya ajali za maji Tanzania

Kadhalika watu wengine 30 wameokolewa wakiwa hai katika ajali hiyo. Hii sio mara ya kwanza kwa Tanzania kushuhudia ajali za majini, ambapo makumi ya watu wamekuwa wakipoteza maisha baharini kwa sababu tofauti zinazovihusisha vyombo vya kusafaria au uzembe wa idara husika.