Amnesty International yataka kuhuishwa mfumo wa sheria Jamhuri ya Afrika ya Kati
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i23320-amnesty_international_yataka_kuhuishwa_mfumo_wa_sheria_jamhuri_ya_afrika_ya_kati
Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty Internatonal) limesema kuwa watenda jinai za kivita yakiwemo mauaji na ubakaji huko Jamhuri ya Afrika ya Kati hawaadhibiwi hatua inayochochea zaidi machafuko nchini humo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jan 12, 2017 04:07 UTC
  •  Amnesty International yataka kuhuishwa mfumo wa sheria Jamhuri ya Afrika ya Kati

Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty Internatonal) limesema kuwa watenda jinai za kivita yakiwemo mauaji na ubakaji huko Jamhuri ya Afrika ya Kati hawaadhibiwi hatua inayochochea zaidi machafuko nchini humo.

Amnesty International imeongeza kuwa makumi ya watu wanaoshukiwa kutenda jinai za kivita na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu wameepa uchunguzi na kutiwa mbaroni na kwamba baadhi ya washukiwa hao wanaishi pamoja na wahanga wa jinai hizo katika nchi ambayo imegawanyika katika makundi ya kikabila na kidini. Ilaria Allegrozzi Mtafiti wa Amnesty International amesema kuwa mfumo wa sheria wa Jamhuri ya Afrika ya Kati umedhoofika.

Walinda amani wa UN wakipiga doria katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui 

Ameongeza kuwa maelfu ya wahanga wa jinai za kivita nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wanasubiri sheria ichukue mkondo wake, huku wale waliotenda jinai za kutisha kama mauaji na ubakaji wakisalia huru. Mtafiti huyo wa Amnesty International ameongeza kuwa mahakama chache zinafanya kazi nje ya mji mkuu Bangui,  na kwamba ni mahakama nane tu kati ya 35 ndizo zinafanya kazi katika nchi nzima huku kukiwa na usalama hafifu unaosababisha jela kadhaa kuvamiwa.