UN yasisitizia udharura wa kukomesha machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati
Umoja wa Mataifa umetangaza azma thabiti uliyonayo ya kukabiliana na hali ya machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Ujumbe wenye majukumu kadhaa wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA umetangaza kuwa, licha ya askari wa kikosi hicho cha kofia buluu kupata hasara mbalimbali, lakini umoja huo umeazimia kukomesha kabisa vyanzo vya machafuko ambayo yamekuwa yakitokea ndani ya taifa hilo la katikati mwa Afrika. Vladimir Monteiro, msemaji wa ujumbe wa MINUSCA nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa, mashambulizi ya hivi karibuni yaliyoambatana na mauaji ya askari watatu wa kofia buluu, hayakuwa na taathira yoyote katika irada ya askari wa kikosi hicho na kwamba, hatua za lazima zinachukuliwa ili kuwabaini wahusika wa hujuma hiyo.
Msemaji wa ujumbe huo amezungumzia pia juhudi kubwa zinazofanywa na askari hao kwa kusihirikiana na jeshi la nchi hiyo kwa ajili ya kuwalinda raia hususan watoto na kuwazuia kutumikishwa na makundi ya wabeba silaha kama askari. Hii ni katika hali ambayo askari hao wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakilaumiwa kwa kushindwa kusimamia amani nchi humo. Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ilikuwa koloni la Ufaransa ilijipatia uhuru mwaka 1960, hata hivyo tangu wakati huo imekuwa ikikumbwa na machafuko yanayotokana na uasi au mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali.