Adama Barrow asema yuko tayari kufanya mazungumzo na Jammeh
Mshindi wa uchaguzi wa Rais nchini Gambia, Adama Barrow amesema yuko tayari kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Rais Yahya Jammeh, ambaye alipinga matokeo hayo.
Barrow amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Jammhe ili kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaiokabili nchi hiyo kwa sasa akisisitiza kuwa, suluhisho la ndani ya nchi ni bora kuliko la nje. Amesema: "Namuomba Jammeh aheshimu madaraka, ningefadhilisha sisi wenyewe hapa nchini tuutafutie ufumbuzi mgogoro uliopo."
Hata hivyo amesisitiza kuwa binafsi amejiandaa kula kiapo cha urais tarehe 19 mwezi huu na wala hakuna jambo litakalosimamisha mpango huo.

Haya yanajiri masaa machache baada Jammeh kusema yuko tayari kufanya mazungumzo na upinzani kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro na mkwamo wa uchaguzi.
Hii ni katika hali ambayo, Bunge la Wawakilishi la Nigeria jana lilipiga kura kuidhinisha uamuzi wa kumpatia hifadhi ya kisiasa Rais Yahya Jammeh wa Gambia endapo atakubali kung'atuka madarakani.
Juhudi za viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi wa Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) za kumshawishi Rais huyo wa Gambia akubali kung'atuka madarakani, hadi sasa bado hazijazaa matunda.