Abdel Fattah el-Sisi katika hatua za kuipiga msasa serikali ya Misri
Hivi karibuni Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri alitangaza kuwa, hivi karibuni ataifanyia marekebisho serikali yake.
Kwa mujibu wa Rais Al-Sisi hivi karibuni taifa la Misri litashuhudia mabadiliko katika muundo wa serikali. Miezi 31 imepita tangu rais huyo aingie madarakani nchini Misri. Hata kama hali ya usalama ya nchi hiyo haiwezi kusemekana kuwa ni shwari hasa baada ya kujiri baadhi ya mashambulizi ya kigaidi, lakini kwa kiasi fulani machafuko ya mitaani hayashuhudiwi sana nchini humo.
Licha ya kwamba waungaji mkono wa harakati iliyopigwa marufuku ya Ikhwanul Muslimin wamekuwa na wasi wasi mkuu juu ya ni namna gani serikali ya Cairo itaamiliana na viongozi na wanachama wa harakati hiyo, lakini wasi wasi huo haujasababisha kutokea machafuko ya mitaani ndani ya taifa hilo la kaskazini mwa Afrika. Hata hivyo isisahulike kuwa, baadhi ya maeneo ya Misri likiwemo eneo la Sinai, yamekuwa yakishuhudia harakati za makundi ya kigaidi.
Pamoja na serikali ya El-Sisi kutekeleza baadhi ya hatua muhimu kama vile ufunguzi wa awamu ya pili ya Kanali ya Suez, iliyofanyika kwa ajili ya kuvutia uungaji mkono wa wananchi, lakini haijafanikiwa kupata uungaji mkono huo. Moja ya sababu kuu zilizosababisha kutokea matatizo ya kiuchumi nchini Misri ni machafuko na ukosefu wa usalama wa ndani katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Misri ilikumbwa na machafuko kati ya mwaka 2011 na 2015. Hii ni katika hali ambayo katika nchi jirani na taifa hilo pia kumeendelea kushuhudiwa machafuko ya kisiasa. Suala hilo limeathiri pakubwa hali ya uchumi wa Misri hususan katika sekta ya utalii ambayo huidhaminia serikali ya Cairo pato kubwa la fedha za kigeni.
Katika kujaribu kupunguza matatizo hayo ya kiuchumi, serikali ya Rais Abdel Fattah el-Sisi ilichukua mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), ingawa hata hivyo shirika hilo liliiwekea masharti magumu ikiitaka kuyafanyia marekebisho baadhi ya mambo kama vile kupunguza kiwango cha ruzuku inayotolewa na serikali nchini. Hali mbaya ya uchumi wa nchi hiyo na kadhalika mashinikizo ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) yaliifanya serikali ya Rais Al-Sisi mwishoni mwa mwaka jana 2016 kupunguza kwa asilimia 50 thamani ya sarafu ya taifa. Utekelezaji wa marekebisho hayo ulioendana na ongezeko la ughali wa bidhaa na huduma za kijamii sanjari na kushuka kwa ruzuku ya serikali kwenye bidhaa muhimu zinazotumiwa sana na wananchi, umewazidishia mashinikizo raia wa taifa hilo.
Matatizo hayo yaliyoibuka katika miezi ya hivi karibuni ndiyo yaliyochochea machafuko na maandamano dhidi ya serikali katika maeneo tofauti ya Misri. Ni kwa ajili hiyo ndipo wataalamu wa mambo wakasema kwamba uamuzi wa Rais Abdel Fattah el-Sisi wa kulifanyia marekebisho baraza lake la mawaziri unahusiana na matatizo ya kiuchumi yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo.