Uchaguzi mdogo wa Bunge Zanzibar, CCM yashinda kiti cha Dimani, yaongoza udiwani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24087-uchaguzi_mdogo_wa_bunge_zanzibar_ccm_yashinda_kiti_cha_dimani_yaongoza_udiwani
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda katika uchaguzi wa ubunge Jimbo la Dimani, Zanzibar na kuzoa viti vya udiwani katika maeneo mengi Tanzania Bara katika majimbo ambayo kura zake zilikuwa zimehesabiwa na matokeo yake kutolewa hadi kufikia jana usiku.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2017 01:21 UTC
  • Uchaguzi mdogo wa Bunge Zanzibar, CCM yashinda kiti cha Dimani, yaongoza udiwani

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda katika uchaguzi wa ubunge Jimbo la Dimani, Zanzibar na kuzoa viti vya udiwani katika maeneo mengi Tanzania Bara katika majimbo ambayo kura zake zilikuwa zimehesabiwa na matokeo yake kutolewa hadi kufikia jana usiku.

Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na vingine vilivyo nje ya umoja huo vimejikuta katika wakati mgumu katika uchaguzi huo mdogo.

CCM iliibuka mshindi katika uchaguzi wa Dimani uliotokana na jimbo kuwa wazi baada ya kifo cha mbunge wake Hafidh Ally Tahri kilichotokea Novemba mwaka jana mjini Dodoma, alikokuwa akihudhuria vikao vya Bunge.

Msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo la Dimani, Fatma Gharib Haji alimtangaza mgombea wa CCM, Juma Ali Juma kuwa mshindi wa ubunge wa jimbo hilo kwa kupata kura 4,860 dhidi ya mpinzani wake Abdulrazak Khatib Ramadhani wa CUF aliyepata kura 1,234.

Uchaguzi mdogo wa Bunge Dimani, Zanznibar

Baadhi ya vyombo vya habari pia vimeripoti kuwa uchaguzi huo mdogo umeshuhudia ghasia na machafuko katika baadhi ya majimbo ya uchaguzi na kwamba polisi wa kuzuia fujo walilazimika kutumia mabomu kwa ajili ya kutuliza ghasia.

Mapema jana Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa chama cha CUF, Salim Bimani alivieleza vyombo vya habari kuwa daftari la wapiga kura lililotumika katika uchaguzi mdogo wa bunge wa jana silo lililotumiwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 na kwamba wapiga kura hewa wengi wamepiga kura katika uchaguzi huo kwa maslahi ya CCM.