Baraza la Mapinduzi la Misri lawataka wananchi wasiitii serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i24137-baraza_la_mapinduzi_la_misri_lawataka_wananchi_wasiitii_serikali
Baraza la Mapinduzi la Misri limewataka wananchi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wasiitii serikali sambamba na maadhimisho ya mapinduzi ya wananchi ya Januari 25, 2011 yaliyomngóa madarakani dikteta Hosni Mubarak.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2017 23:26 UTC
  • Baraza la Mapinduzi la Misri lawataka wananchi wasiitii serikali

Baraza la Mapinduzi la Misri limewataka wananchi wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wasiitii serikali sambamba na maadhimisho ya mapinduzi ya wananchi ya Januari 25, 2011 yaliyomngóa madarakani dikteta Hosni Mubarak.

Shirika la habari la ISNA limelinukuu baraza hilo ambalo ni mpinzani mkubwa wa mapinduzi ya kijeshi yaliyomngóa madarakani Muhammad Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa na wananchi nchini Misri, likiwataka wananchi wa nchi hiyo kumiminika mabarabarani kwa lengo la kuonesha hasira zao kutokana na ukandamizaji unaofanywa na serikali ya nchi hiyo.

Maha Izam, mkuu wa Baraza la Mapinduzi la Misri amesema, mapinduzi ndiyo njia pekee ya kukabiliana na serikali inayoungwa mkono na jeshi huko Misri na ambayo inaendeleza udikteta nchini humo. 

Mwito huo wa Baraza la Mapinduzi la Misri umetolewa mbele ya waandishi wa habari katika mji wa Istambul nchini Uturuki na kuhudhuriwa na wanasiasa na wabunge wa zamani wa Misri.

Wananchi wa Misri katika maandamano

 

Kesho Jumatano ni siku ya kuadhimisha mwaka wa sita wa mapinduzi ya Januari 25, 2011 ambapo wananchi wa Misri walioandamana katika kila kona ya nchi hiyo, walifanikiwa kumngóa madarakani dikteta Hosni Mubarak, ambaye alikuwa mkandamizaji na kibaraka mkubwa wa nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hata hivyo miaka miwili baadaye, yaani mwaka 2013, jeshi la Misri lilifanya mapinduzi mengine yaliyomngóa madarakani Muhammad Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo na baadaye kuitishwa uchaguzi wa kimaonesho uliomuweka madarakani Jenerali Abdul Fattah el Sisi, rais wa hivi sasa wa Misri.