UN: Hali ya usalama CAR inatia wasi wasi mkubwa
Umoja wa Mataifa umeonyesha wasi wasi wake mkubwa kufuatia kuendelea machafuko katika baadhi ya maeneo ya katikati mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Taarifa iliyotolewa na Michel Yao, mkuu wa ofisi ya uratibu wa masuala ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa nchini humo (OCHA) imesema kuwa, mapigano yanayoendelea baina ya makundi ya wabeba silaha katika mji wa Bambari, yamekwamisha shughuli za ufikishaji misaada ya kibinaadamu kwa raia.
Kufuatia hali hiyo, Michel Yao ameyataka makundi ya wabeba silaha kusimamisha haraka mapigano na kupisha shughuli za kibinaadamu kwa wakazi wa mji huo. Amesisitiza kuwa, hadi sasa jumla ya wakazi laki sita wa mji wa Bambari wanakabiliwa na hali mbaya sana ya kimaisha na usalama kutokana na mapigano hayo.
Mkuu huyo wa ofisi ya uratibu wa masuala ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa nchini humo (OCHA) ameongeza kuwa, hali ya usalama wa katikati mwa nchi hiyo ikiwa ni hiyo, maeneo mengine nayo hayajasalimika na machafuko hayo.
Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoka madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, François Bozizé, huku mgogoro ukishadidi zaidi baada ya waasi wa Kikristo wenye kufurutu ada wa Anti-Balaka kuanzisha mauaji ya kutisha dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.