Mali yaonyesha hamu ya kuimarisha uhusiano na Iran
Rais wa Bunge la Kitaifa la Mali amesisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano wa pande mbili kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Issaka Sidibe, Rais wa Bunge la Taifa la Mali aliyasema hayo jana Jumapili wakati akiuaga ujumbe wa maafisa wa ngazi za juu wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) walioitembelea nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Ujumbe huo uliongozwa na Kazem Jalali, ambaye pia ni Mkuu wa Kituo cha Utafiti cha Bunge la Iran.
Sidibe amepongeza nafasi na mchango wa Iran katika Kongamano la 12 la Umoja wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu IPU, lililomaliza shughuli zake Jumamosi mjini Bamako nchini Mali akisisitiza kuwa, anatumai mkutano huo utasaidia kuimarisha umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu.
Kwa upande wake, Kazem Jalali, Mkuu wa Kituo cha Utafiti cha Bunge la Iran amepongeza ukarimu wa Mali na juhudi zake za kuhakikisha kuwa kongamano hilo linakuwa la kufana. Ameongeza kuwa, Tehran na Bamako zitaendeleza mazungumzo yao ya mara kwa mara kwa shabaha ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika nyuga tofauti.
Mkutano huo wa Umoja wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu ambao ulianza Jumatatu iliyopita, mbali na kujadili changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu, pia uligusia masuala ya kuimarisha demokrasia, usalama, amani na uthabiti katika nchi za Kiislamu.
Januari 11 akiwa hapa mjini Tehran, Rais wa Bunge la Kitaifa la Mali alisema msimamo wa nchi yake kuhusu kadhia ya Palestina unafanana na wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku akikashifu mienendo ya Umoja wa Mataifa dhidi ya taifa hilo la Kiarabu kwa miaka kadhaa sasa.