Daesh yadai imeua na kujeruhi wanajeshi 20 wa Misri, Sinai
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limedai kwamba limeua na kujeruhi wanajeshi 20 wa Misri kaskazini mwa eneo la Sinai.
Taarifa ya kundi hilo la kigaidi imesema kuwa, zaidi ya askari 20 wa Misri wameuawa na kujeruhiwa katika makabiliano ya siku nne na wanachama wa kundi hilo katika mji wa al-Arish, kaskazini mwa eneo la Sinai.
Shirika la habari la AP limesema kuwa, serikali haijatoa taarifa kukiri au kukanusha madai hayo ya magaidi wa Daesh, na waandishi wa habari hawana taarifa za ziada kwa kuwa Peninsula ya Sinai haiendeki kutokana na ukosefu wa usalama na makabiliano ya mara kwa mara kati ya vikosi vya serikali na wanachama wa Daesh.
Taarifa ya Daesh imeongeza kuwa, mbali na kuua na kujeruhi wanajeshi wa Misri, kundi hilo la kigaidi limefanikiwa kusambaratisha magari kadhaa ya kijeshi katika eneo hilo.
Mwezi uliopita, magaidi wanaofungamana na kundi la kigaidi la ISIS au Daesh nchini Misri waliua raia 16 huko Sinai kwa tuhuma za kushirikiana na jeshi la serikali. Kabla ya hapo, askari 8 waliuawa katika shambulio la bomu huko Sinai, kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Hali ya hatari ilitangazwa katika eneo hilo la Sinai mwaka 2014, baada ya wanajeshi 30 kuuawa katika shambulizi jingine la kigaidi.