Kongamano la wafuasi wa dini kuishi kwa masikilizano lafanyika UDSM, Tanzania
Kongamano la wafuasi wa dini mbalimbali kuishi kwa masikilizano na utumiaji wa akili na mantiki kwa mtazamo wa mafundisho ya Imam Ridha (as) limefanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania.
Kongamano hilo ambalo lilifanyika jana sambamba na kuwadia maadhimisho ya Alfajiri Kumi ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran limeandaliwa kwa ushirikiano wa Kituo cha Kiutamaduni cha Iran nchini Tanzania, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Baraza la Dini kwa ajili ya Amani na kwa msaada na uungaji mkono wa Taasisi ya Kimataifa ya Utamaduni ya Imam Ridha (as).
Akihutubia katika kongamano hilo, Rose Muzala, Mkuu wa Kitivo cha Sayansi za Jamii cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema, dini bila ya akili na mantiki ina madhara, na akili tupu bila ya dini haina ufanisi. Aidha ametoa shukurani kwa kituo cha Kiutamaduni cha Iran nchini Tanzania.
Mussa Farhang, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania ambaye alikuwa mzungumzaji mwengine katika kongamano hilo, amesema kuishi kwa masikilizano wafuasi wa dini mbalimbali katika Jamhuri ya Kiislamu kuna chimbuko la kihistoria; na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umejumuisha pamoja dini na akili.
Mbali na kupongeza hali ya kuishi kwa masikilizano iliyopo baina wa waumini wa dini mbalimbali nchini Tanzania, Farhang ameongeza kuwa hitilafu za kidini ni jambo la kawaida, lakini inachopasa kufanya ni kutilia mkazo nukta za pamoja badala ya hitilafu.
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania amesisitiza kuwa wanaofanya jinai kwa jina la dini ni watu wasio na akili timamu; na njia pekee ya kuwezesha wafuasi wa dini tofauti kuishi kwa masikilizano ni kujiepusha na vitendo vya machafuko na ukatili.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Zanzibar, Rashid Ali Juma, yeye ameashiria historia ya pamoja ya Iran na Tanzania na kusisitiza azma ya Zanzibar ya kuimarisha uhusiano baina ya pande mbili.
Kongamano hilo limehudhuriwa pia na wahadhiri pamoja na wanachuo wa nchini Tanzania…/