Mkakati wa Misri wa kuasisi Umoja wa kaskazini mwa Afrika
Misri imesema inataka kuanzisha Umoja wa Kaskazini mwa Afrika.
Sameh Shoukry Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amependekeza mipango kadhaa na masuala ya pamoja na kieneo ukiwemo mpango wa kuanzisha Umoja huko Kaskazini mwa Afrika utaofahamika kwa jina hilo kwa kuzishirikisha nchi za Kiarabu na zisizo za Kiarabu. Shoukry ameyasema hayo katika mazungumzo na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Algeria, Nigeria na Jamhuri ya Kongo pambizoni mwa kikao cha AU huko Addis Ababa, Ethiopia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri pia amebainisha kuwa hivi karibuni atafanya kikao na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za kaskazini mwa Afrika huko Cairo ili kuzungumzia masuala hayo. Misri imewasilisha pendekezo hilo katika hali ambayo nchi za kaskazini mwa Afrika kila moja inakabiliwa na matatizo mengi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Hata kama nchi kama Misri na Tunisia zimepitia kipindi cha kisiasa kwa nchi hizo kuwa na tajiriba ya miamko ya Kiislamu, lakini hazijafanikiwa kurejesha uthabiti na usalama unaotakiwa; huku wananchi wakiandamana dhidi ya serikali kupinga masuala mbalimbali. Sudan nayo inakabiliwa na maandamano na matatizo ya kisiasa. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi nyingine za eneo pia zinakabiliwa na migogoro na mizozo mbalimbali ya ndani na hata kama hadi sasa kumefikiwa muafaka wa kupatiwa suluhu matatizo hayo, lakini bado masuala mengi makuu hayajapatiwa ufumbuzi. Katika upande mwingine, suala la wahamiaji, kurejea magaidi, mgogoro wa kisasa huko Libya ni miongoni mwa matatizo yanayolikabili eneo la kati na kaskazini mwa Afrika.
Umoja wa Afrika ukiwa taasisi ya kibara ambayo imekuwa na nguvu ya kiasi fulani kwa miaka kadhaa sasa inafanya kila iwezalo kuyakabili matatizo ya nchi za bara hilo. Umoja wa Afrika kwa kiwango fulani umefanikiwa kudhibiti hali ya mambo kupitia juhudi zake za upatanishi au kutumia njia nyingine za ufumbuzi kutatua migogoro katika nchi za Kiafrika. Katika mazingira hayo, lengo la Misri la kuwasilisha pendekezo la kutaka kuanzisha Umoja wa Kaskazini mwa Afrika linaweza kuakisiwa kwa pande kadhaa. Kwa upande mmoja, pendekezo la Misri linaweza kuhusishwa na matukio ya kieneo. Kwa kuzingatia matukio ya kieneo inaonekana kuwa, Misri inataka kutetea nafasi yake kuu yenye taathira katika mchakato wa matukio yanayojiri katika eneo. Hasa ikitiliwa maanani kuwa, kabla ya hapo na katika zama za vita baridi na hususan wakati wa vita kati ya Waarabu na Israel, Misri ilikuwa na nafasi ya kiuongozi na ilisimamia mirengo ya kisiasa katika eneo. Hata hivyo nchi hiyo sasa haina tena ushawishi na uwezo huo wa huko nyuma; na ndio maana inafanya kila iwezalo ili iwe na nafasi huko kaskazini mwa Afrika japokuwa ya kiwango fulani kwa kuzishawishi nchi nyingine ili kuasisi Umoja wa Kieneo wa nchi za kaskazini mwa Afrika. Katika upande mwingine ni kuwa, kwa kuzingatia mvutano uliopo katika uhusiano kati ya Misri na Saudi Arabia kuhusu masuala ya kieneo ikiwemo kadhia ya Syria. inaonekana kuwa Cairo inafanya jitihada za kuasisi muungano ili kutekeleza harakati sawa kabisa na zile za Saudi Arabia. Mpango wa kuasisi Umoja wa kaskazini mwa Afrika unaweza kwa kiwango fulani kuiwezesha Misri kufikia lengo lake hilo.