Jeshi la Misri laangamiza magaidi 14 katikati mwa Sinai
Jeshi la Misri limewaangamiza magaidi 14 katika mkoa wa Sinai na kuwatia mbaroni wengine kumi kufuatia operesheni kali ya jeshji la nchi hiyo katika maeneo hayo.
Kanali Tamer al-Rifai, msemaji wa jeshi la Misri ameziambia duru za habari kwamba, jeshi la nchi hiyo limeendesha operesheni ya siku tano ambapo limefanikiwa kuangamiza magari matatu yaliyokuwa yametegwa mabomu ndani yake na kukamata vifaa na zana mbalimbali za kijeshi.
Aidha ripoti zinasema kuwa, jeshi la Misri limefanikiwa kutokomeza maficho ya kundi la wabeba silaha katikati mwa mkoa wa Sinai na kufanikiwa kukamata kiwango kikubwa cha silaha, vyombo vya mawasiliano ya kijeshi na magwanda ya kijeshi.
Eneo la Sinai limekuwa likishuhudia mauaji mara kwa mara kutokana na kuweko makundi kadhaa ya wabeba silaha yanayoendesha harakati zao katika maeneo ya mkoa huo ambapo kundi muhimu zaidi ni la Wilaya ya Sinai.
Kundi hilo ambalo zamani likijulikana kama Ansar Bait al Maqdis mwaka 2014 lilitangaza utiifu kwa kundi la kigaidi la Daesh ndilo ambalo limekuwa likitekeleza hujuma na mashambulio ya mara kwa mara huko Sinai dhidi ya raia na maafisa usalama katika eneo hilo.
Tangu wakati huo jeshi la Misri limepiga kambi kaskazini mwa nchi hiyo kwa ajili ya kupambana na wanamgambo hao ambao wamekuwa wakifanya mashambulizi ya kigaidi mara kwa mara.