Viongozi wa nchi za Sahel Afrika wasisitiza mapambano dhidi ya ugaidi
Viongozi wa nchi tano za eneo la Sahel barani Afrika wametilia mkazo udharura wa kuwepo ushirikiano na kuchukuliwa hatua za haraka za kupambana na ugaidi na makundi yenye misimamo mikali katika eneo hilo.
Mwishoni mwa mkutano wao uliofanyika Bamako nchini Mali, viongozi wa nchi tano za Burkina Baso, Mali, Mauritania, Niger na Chad zinazounda kundi la G5 Sahel, wamekubaliana kushirikiana na kuchukua hatua za haraka kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Mkutano huo wa Bamako umefanyika mwezi mmoja tu baada ya mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 18 Januari katika mji wa Gao huko kaskazini mwa Mali ambayo yaliua watu wasiopungua 77.
Rais Idriss Déby wa Chad amesema kuwa makundi ya kigaidi yanafanya mikakati ya kuzitumbukizi nchi za Afrika katika vita ngumu na ya muda mrefu.
Mwenyeji wa mkutano wa Bamako, Rais Ibrahim Boubacar Keïta wa Mali amesema nchi za Afrika zinapaswa kushirikiana na kuratibu mipango yao katika juhudi za kupambana na makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka na ya kigaidi.
Viongozi wa nchi 5 za Sahel pia wamekubaliana kuanzisha makao makuu ya kikosi cha kupambana na ugaidi huko kaskazini mwa Mali eneo ambalo linatumiwa na makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka kwa ajili ya kutuma magaidi katika nchi nyingine za Kiafrika.