Wakulima Wazungu wanakabiliwa na njaa nchini Zimbabwe
Kwa akali wakulima 1000 Wazungu wanakabiliwa na hali mbaya ya njaa nchini Zimbabwe kutokana na kile kinachotajwa kuwa sera ya kibaguzi ya ardhi.
Michael Carter, Seneta wa chama cha MDC amesema mpango wa kuzifanyia marekebisho sera za ardhi nchini Zimbabwe ulioanza kutekelezwa mwaka 2000, umesababisha wakulima Wazungu zaidi ya 1000 nchini humo waendelee kupitia kipindi kigumu cha njaa. Amesema: "Sera hiyo ni ya kibaguzi na inayokiuka katiba ya nchi. Ubaguzi huo ni sawa na ule wa serikali ya Smith dhidi ya watu weusi, na naamini kuwa, kufanya makosa mawili hakufanyi jambo likawa sawa", amesisitiza Seneta Michael Carter.
Taathira hasi za El-nino na ukame vimeifanya Zimbabwe ikumbwe na upungufu mkubwa wa chakula kwa kadiri kwamba hivi sasa kati ya watu milioni tatu hadi nne wa nchi hiyo wanahitajia misaada ya dharura ya chakula.
Wakosoaji wa Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo wanasema kuwa kiongozi huyo amefeli katika siasa zake za kuwapa wenyeji mashamba yaliyokuwa yamehodhiwa na Wazungu. Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, siasa hizo zimepelekea kupungua sana mazao ya kilimo kama vile mahindi.
Ikumbukwe kuwa, mapema mwaka 2000, Rais Mugabe alianza kutekeleza siasa za marekebisho ya ardhi akisema kuwa, Wazungu walio wachache wamehodhi sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba ya nchi hiyo na kuwanyima wenyeji haki yao ya kufaidika na neema na rasilimali za nchi yao.