Kikosi cha UN Jamhuri ya Afrika ya Kati kutiwa nguvu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25294-kikosi_cha_un_jamhuri_ya_afrika_ya_kati_kutiwa_nguvu
Umoja wa Mataifa umeamua kukitia nguvu kikosi cha askari buluu cha umoja huo kinacholinda amani katika maeneo ya katikati mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 18, 2017 04:11 UTC
  • Kikosi cha UN Jamhuri ya Afrika ya Kati kutiwa nguvu

Umoja wa Mataifa umeamua kukitia nguvu kikosi cha askari buluu cha umoja huo kinacholinda amani katika maeneo ya katikati mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Parfait Onanga-Anyanga, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema, umoja huo utatuma askari wake katika maeneo ya katikati mwa nchi hiyo ukiwemo mji wa Bambari ili kulisaidia jeshi la CAR kuwalinda raia kutokana na kuongezeka machafuko kwenye maeneo hayo katika siku za hivi karibuni.

Shirika la habari la Xinhua limemnukuu Parfait Onanga-Anyanga akiongeza kuwa, mji wa Bambari haupaswi kuachiliwa kuwa mikononi mwa makundi yenye silaha, hivyo Umoja wa Mataifa utaelekeza nguvu zake kwenye kuwafurusha watu wenye silaha mjini humo.

Amesema, askari kutoka Bangladesh watatumwa Jamhuri ya Afrika ya Kati kukitia nguvu kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.

Machafuko Jamhuri ya Afrika ya Kati limekuwa ni jambo la kawaida

Harakati ya Umoja kwa ajili ya Amani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (UPC) na Kikosi cha Wananchi kwa Ajili ya Kuihuisha Jamhuri ya Afrika ya Kati (FPRC) ni makundi mawili yenye silaha ambayo yanahesabiwa ni tishio kubwa kwa usalama wa nchi hiyo.

Tangu mwaka 2013, Jamhuri ya Afrika ya Kati imekumbwa na mapigano makali ya ndani yaliyopelekea kuharibika miundombinu na maafa makubwa kwa raia wakiwemo Waislamu.