kuongezeka ushirikiano baina ya Uingereza na Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i25676-kuongezeka_ushirikiano_baina_ya_uingereza_na_misri
Ikiwa ni katika juhudi za Uingereza za kupanua mahusiano yake na nchi nyingine, Boris Johnson, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo amefanya safari nchini Misri kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa pande mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2017 23:14 UTC
  • kuongezeka ushirikiano baina ya Uingereza na Misri

Ikiwa ni katika juhudi za Uingereza za kupanua mahusiano yake na nchi nyingine, Boris Johnson, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo amefanya safari nchini Misri kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa pande mbili.

Akizungumza mjini Cairo, mji mkuu wa Misri na Rais Abdel Fattah el-Sisi na Sameh Shoukry, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Boris Johnson amesisitiza kuwa, Misri ina nafasi mihimu sana katika kuimarisha usalama na uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati.  Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amesema kuwa, London iko mstari wa mbele katika kuunga mkono harakati za marekebisho nchini Misri na kudai kuwa, hiyo ni kwa kuwa suala hilo linasaidia kuimarisha usalama na maendeleo ya eneo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Boris Johnson kushoto akiwa na waziri mwenza wa Misri

Hata kama safari ya Johnson nchini Misri inatajwa kuwa yenye lengo la kuongeza mahusiano ya kiuchumi, sambamba na kusisitizia udharura wa mashirikiano katika kupambana na ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati, lakini ziara ya Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Uingereza katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inatajwa kuwa na malengo mengine ya siri. Hii ni kwa kuwa, hatua ya Uingereza ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, imeifanya London kuimarisha zaidi mahusiano na nchi tofauti kuliko wakati mwingine wowote ule hususan na makoloni yake ya zamani pamoja na nchi zinazoshuhudia mabadiliko mapya ya kisiasa.

Hali ya umasikini nchini Misri

Hivi sasa London imeingia katika ushindani wa siri na wa wazi na nchi nyingine za Magharibi ikiwemo Marekani, hivyo kuongeza mahusiano yake na baadhi ya nchi kama vile Misri, kunafanyika katika fremu hiyo. Kwa kuzingatia kuwa Misri imejiimarisha katika mlingano wa kisiasa katika eneo, Uingereza imekuwa ikifanya juhudi za kupenyeza ushawishi wake ndani ya nchi hiyo, kuelekea eneo zima la Mashariki ya Kati na nchi za Kiarabu. Ni kwa msingi huo ndio maana Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, akafanya safari mjini Cairo na kusisitizia umuhimu wa kuimarishwa mahusiano ya pande mbili.

Hii ni katika hali ambayo Misri pia sambamba na kushuhudia mabadiliko tofauti ya kisiasa na kijamii hususan baada ya harakati ya mwamko wa Kiislamu, hivi sasa inakusudia kupanua ushawishi wake katika eneo kwa kuwajumuisha marafiki zake ili kwa mara nyingine tena iweze kuhuisha nguvu na nafasi yake ya zamani katika eneo. Hayo yanajiri huku nchi hiyo ikiwa inakabiliwa na matatizo ya ndani ya kiuchumi na kiusalama. Katika fremu hiyo, sekta yake ya utalii imekumbwa na matatizo makubwa kufuatia migogoro ya ndani na hivyo kutoa pigo kubwa kwa pato lake la fedha za kigeni.

Mashambulizi ya kigaidi yanayoikabili Misri hivi sasa

Ukosefu wa ajira, umasikini na migogoro ya kijamii ni mambo mengine yaliyoshadidi nchini Misri, huku viongozi wa Cairo wakiwa wameshindwa kubuni mipango ya maana kwa ajili ya kuyatatua na kuboresha hali ya uchumi. Aidha viongozi hao wameshindwa kubuni nafasi za ajira na kuzuia ongezeko la umasikini na badala yake Cairo imejikita katika kuboresha mahusiano na madola ya Magharibi kama inavyoshuhudiwa katika safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza ambapo pande mbili zimetiliana saini makubaliano ya kuipatia Misri mkopo wa dola milioni 150.

Udhamini huo wa kibenki unajumuisha pia msaada wa dola bilioni 12 kutoka Shirika la Fedha Duniani IMF kwa Misri ambao makubaliano yake yalifikiwa mwezi Novemba uliopita. Kwa upande mwingine ni kwamba, hata kama serikali ya Cairo imeweza kupiga hatua kwa kiasi fulani, lakini migogoro ya majirani na nchi hiyo ikiwemo Libya imepelekea kuongezeka makundi ya kigaidi suala ambalo limewakosesha amani viongozi wa serikali hiyo. Ni kwa ajili hiyo ndio maana katika safari hiyo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, kukajadiliwa njia za namna ya kupambana na tatizo hilo.

Magaidi wa Kiwahabi wenye mafungamano na genge la Daesh wakifanya mazoezi Sinai, Misri

Inaonekana kuwa safari ya Boris Johnson nchini Misri na katika mazingira ya sasa ni fursa muhimu kwa pande mbili kufuatilia kwa karibu maslahi yao. Hii ni kusema kuwa katika safari hiyo Uingereza inachuana na madola ya Magharibi nchini Misri huku kwa upande wake Misri nayo ikiwa inaitazama safari hiyo kama fursa ya kutatuliwa matatizo yake ya kiuchumi na wakati huo huo kuinua ushawishi  wake katika eneo la Mashariki ya Kati.