Watu wasiopungua 30 wauawa katika mapigano kusini mwa Tunisia
Watu wasiopungua 30 wameuawa katika mapigano kati ya vikosi vya jeshi la Tunisia na magaidi yaliyotokea kwenye mji Ben Guerdan ulioko karibu na mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Libya.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imetangaza kuwa wanamgambo wenye silaha leo asubuhi walishambulia vituo vya ukaguzi vya jeshi na polisi katika eneo hilo. Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa wanamgambo 21 wameuliwa na wengine sita wametiwa nguvuni katika mapigano hayo.
Shambulio la leo asubuhi ni la pili la umwagaji damu kufanywa na magaidi katika kipindi cha wiki moja katika maeneo ya mpakani mwa Tunisia.
Duru za hospitali zimeripoti kuwa raia wasiopungua watano akiwemo mtoto mdogo mwenye umri wa miaka mitatu na mwengine wa kiume mwenye umri wa miaka 12 pamoja na askari mmoja pia waliuawa katika mapigano hayo.
Kufuatia mapigano ya leo, maafisa wa serikali ya Tunis wametangaza marufuku ya kutotoka nje na kuwataka wakaazi wa mji huo wa Ben Guerdan wabaki majumbani mwao.
Msemaji wa jeshi la Tunisia ametangaza kuwa baada ya mapigano hayo magaidi waliosalia walikimbia kuelekea mpaka wa Libya. Ameongeza kuwa hali ya mambo mjini humo iko chini ya udhibiti na kwamba vikosi vya usalama vinaendelea kuwasaka magaidi hao.
Tunisia imekuwa kila mara ikikabiliwa na tishio la makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao katika nchi jirani ya Libya. Raia kadhaa wa Tunisia wamejiunga na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh; na magenge kadhaa yenye mfungamano na kundi hilo yameshatiwa mbaroni.../