Waliouawa kwa kimbunga Madagascar wafikia 38
Watu wasiopungua 38 wameuawa kwa kimbunga cha "Enawo" kilichoikumba Madagascar wiki hii. Hayo yameelezwa na afisa wa Idara ya Kukabiliana na Majanga ya nchi hiyo.
Thierry Venty amesema kuwa, watu 38 wamefariki dunia kwa kimbunga hicho kilichoiathiri Madagascar ikiwemo familia nzima iliyopoteza maisha kutokana na maporomoko ya udongo. Watu wengine wanaokadiriwa kuwa 153,000 wameachwa bila ya makazi.
Kimbunga cha Enawo Jumanne iliyopita kililikumba eneo la pwani ya kaskazini mashariki mwa Madagascar, eneo linalozalisha zao la vanilla na kubomoa barabara na kukata njia za mawasiliano katika wilaya ya Antalaha yenye idadi ya watu 230,000.
Watu zaidi ya 116,000 wameathiriwa moja kwa moja na kimbunga hicho. Idara ya Hali ya Hewa ya Madagascar imetangaza kuwa, kimbunga cha "Enawo" kimepungua makali yake kwa kuwa na mawimbi ya kasi ya kilomita 45 hadi 50 kwa saa.