Iran yakaribishwa kuwekeza katika usindikaji bidhaa Tanzania
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeikaribisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwekeza katika sekta ya viwanda nchini humo, hususan katika viwanda vya kusindika bidhaa.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu wa Tanzania imemnukuu Kassim Majaliwa akisema: “Tumedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda, tunawakaribisha wawekezaji kutoka Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo na uvuvi.”
Kauli hiyo ya Waziri Mkuu wa Tanzania ilitolewa katika mazungumzo ya jana baina yake na Balozi wa Iran nchini humo.
Waziri Mkuu Majaliwa pia amesema, Tanzania inawakaribisha raia wa Iran kuitembelea Tanzania kama watalii kwa sababu kuna fursa nyingi za utalii.
Ikumbukwe kuwa uhusiano wa kihistoria baina ya Iran na nchi za Afrika Mashariki ni wa muda mrefu sana.
Kwa upande wake, Mousa Farhang, Balozi wa Iran nchini Tanzania amesema anaishukuru nchi hiyo kwa ushirikiano mzuri na Tehran na ameiomba ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo, ambapo Waziri Mkuu wa Tanzania amekubali.
Vile vile amesema, Tanzania na Iran zina uhusiano wa kihistoria ambao unadhihirishwa na uwepo wa Washirazi wengi husan visiwani Zanzibar ambao wana asili ya Iran kama ambavyo amesema, katika maeneo ya kusini mwa Iran pia kuna watu wengi wenye asili ya Afrika ambao hata muonekano wao ni wa Kitanzania.