UN yalalamikia ongezeko kubwa la uvunjaji wa haki za binadamu DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i26748-un_yalalamikia_ongezeko_kubwa_la_uvunjaji_wa_haki_za_binadamu_drc
Mjumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa amelalamikia vikali ongezeko la uvunjaji wa haki za binadamu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 23, 2017 03:31 UTC
  • UN yalalamikia ongezeko kubwa la uvunjaji wa haki za binadamu DRC

Mjumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa amelalamikia vikali ongezeko la uvunjaji wa haki za binadamu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akizungumza kwenye kikao cha baraza hilo kilichokutana jana mjini Geneva Uswisi kwa ajili ya kujadili hali ya ukosefu wa amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Andrew Gilmour amesema, kiwango cha uvunjaji wa haki za binadamu mwaka 2016 nchini Kongo kiliongezeka kwa asilimia 30.

Naye Maman Sidikou, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesisitiza kuwa, matukio ya kisiasa na kiusalama ya miezi ya hivi karibuni yameambatana na uvunjaji wa haki za binadamu nchini humo.

Msafara wa wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 

 

Mgogoro wa kisiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliongezeka baada ya kuakhirishwa uchaguzi wa rais na pia kutokana na hatua ya Rais Kabila ya kungángánia kubakia madarakani licha ya muda wake wa kutawala kumalizika.

Siku chache zilizopita kulitolewa mikanda zaidi ya video za mauaji yanayodaiwa kufanywa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dhidi ya raia wa nchi hiyo suala ambalo limezua kashfa mpya dhidi ya serikali. 

Mikanda hiyo iliyoenea kwenye mitandao ya kijamii, inawaonesha wanajeshi wa serikali ya Congo wakiwaua kikatili wanachama wa kundi la Kamuina Nsapu katika mkoa wa Kasai. Moja ya mikanda hiyo ya video ambao ulichukuliwa mwezi Januari mwaka huu unaonesha picha za kaburi la umati lililogunduliwa katika eneo la Kasai huko Kongo.