Rais wa Gabon azindua mazungumzo ya amani, Ping asusia
(last modified Wed, 29 Mar 2017 02:56:04 GMT )
Mar 29, 2017 02:56 UTC
  • Rais wa Gabon azindua mazungumzo ya amani, Ping asusia

Rais Ali Bongo wa Gabon amezindua mazungumzo yanayoyaleta pamoja makundi ya kisiasa nchini humo kwa shabaha ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa, kiuchumi na kijami uliotokana na matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana.

Makundi 1,200 ya kisiasa na kijamii yanashiriki mazungumzo hayo yaliyozinduliwa hapo jana na Rais Bongo, vikiwemo vyama 50 vya siasa, maafisa wa serikali na wanadiplomasia.

Hata hivyo hasimu wa kisiasa wa Rais Ali Bongo, Jean Ping amesusia mazungumzo hayo. Itakumbukwa kuwa mwanadiplomasia huyo ambaye alikuwa mgombea wa upinzani katika uchaguzi wa rais wa Agosti mwaka jana 2016, alipinga matokeo hayo yaliyomtangaza mshindi Ali Bongo.

Mbali na kupinga matokeo hayo na kupinga wito wa mazungumzo, Ping alituma faili la mashtaka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kulalamikia vitendo vya utumiaji mabavu anavyodai vinafanywa na serikali ya nchi hiyo dhidi ya wapinzani na wakosoaji.

Mwanadiplomasia Jean Ping

Akihutubu katika uzinduzi wa mazungumzo hayo jana Jumanne mjini Libreville, Rais wa Gabon alisema mgogoro unaoikumba nchi hiyo kwa sasa, ni sawa na mzozo wa kifamilia na kusisitiza kuwa mgogoro huo haujaanza sasa bali umelikumba taifa hilo kwa muda mrefu hata kabla ya kujipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa mwaka 1960.

Bongo amesema mazungumzo hayo yatakayodumu kwa muda wa wiki tatu yatajadili masuala nyeti kama vile mageuzi katika taasisi za umma, kufanyiwa marekebisho mfumo wa uchaguzi, kutazamwa upya majukumu ya Mahakama ya Katiba na kujadili mikakati ya kuimarisha amani na utangamano wa kijamii.

Licha ya serikali kutangaza kuwa watu watatu pekee ndio waliouawa katika machafuko ya baada ya uchaguzi huo wa Agosti mwaka jana, vyama vya upinzani vimekuwa vikishikilia kuwa ni watu zaidi ya 50 waliuawa, mbali ya wengine 1000 kukamatwa na polisi.