Malengo ya safari ya Waziri Mkuu wa Ufaransa barani Afrika
Waziri Mkuu wa Ufaransa Bernard Cazeneuve ameanza safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika ambayo imetajwa kuwa lengo lake ni kuimarisha uchumi na mapambano dhidi ya ugaidi.
Bernard Cazeneuve aliwasili jana alasiri nchini Algeria na kulakiwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abdelmalek Sellal. Cazeneuve pia atakutana na Rais wa Algeria na kubadilishana naye mawazo kuhusu ushirikiano wa pande mbili hususan katika nyanja za kupambana na ugaidi na masuala kiuchumi.
Safari ya Bernard Cazeneuve nchini Algeria ni ya tano kufanywa na kiongozi huyo nchini humo katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Francois Hollande wa Ufaransa. Mbali na maudhui ya ugaidi, masuala mengine yanayojadiliwa na pande hizo mbili ni tatizo la wahajiri haramu, mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi na sekta ya viwanda. Baada ya Algeria, Waziri Mkuu wa Ufaransa anatarajiwa kuelekea katika nchi jirani ya Tunisia.
Japokuwa historia ya ukoloni wa Ufaransa katika nchi za kaskazini mwa Afrika inarejea miaka mingi huko nyuma na aghlabu ya nchi za eneo hilo hususan Algeria ziliweza kujikomboa kutoka kwenye makucha ya mkoloni huyo kwa mapambano ya muda mrefu na mashaka makubwa, lakini nchi za kikoloni za Magharibi ikiwemo Ufaransa, zingali zinataka kuwepo kwa njia moja au nyingine barani Afrika; na katika uwanja huo zinatumia siasa mpya za ukoloni mamboleo na kwa kutumia miavuli yenye rangi za aina mbalimbali kama vile misaada ya kijeshi, uwekezaji wa kiuchumi na kadhalika.
Katika uwanja huu nchi za kaskazini mwa Afrika hususan Algeria na Tunisia daima zimekuwa na umuhimu mkubwa kwa Ufaransa, na maafisa wa serikali ya Paris wanafanya mikakati ya kupenya na kuwa na ushawishi katika nchi hizo kwa kutumia visingizio mbalimbali. Safari ya sasa ya Waziri Mkuu wa Ufaransa huko kaskazini mwa Afrika inafanyika katika kipindi ambacho suala la ugaidi na kupambana na janga hilo limekuwa tatizo kubwa si kwa Ufaransa pekee bali kwa bara zima la Ulaya. Janga hilo ambalo ni matokeo ya siasa za nchi za Magharibi za kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine sasa limekuwa hatari kwa nchi hizo zenyewe. Hivyo, ili kuweza kudhibiti hali hiyo, Ufaransa inahitajia ushirikiano wa nchi za kaskazini mwa Afrika hususan Algeria na Tunisia mbazo ni nchi muhimu zenye mipaka ya pamoja na nchi ya Libya. Suala hilo pia limetiliwa mkazo na Bernard Cazeneuve mwenyewe aliposema, kuna udharura mkubwa wa kuwepo ushirikiano kati ya Ufaransa na nchi za kusini mwa Bahari ya Mediterania hususan Algeria na Tunisia katika kupambana na ugaidi.
Hali ya mambo nchini Libya baada ya kuondolewa madarakani utawala wa Muammar Gaddafi na machafuko ya ndani nchini humo vimetayarisha mazingira ya kustawi makundi ya kigaidi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na hatari hiyo inahisika vyema katika nchi mbalimbali duniani.
Masuala ya kiuchumi na kiviwanda ni kati ya mambo yanayopewa kipaumbele katika safari ya sasa Waziri Mkuu wa Ufaransa katika nchi za Algeria na Tunisia. Suala hilo linapata umuhimu zaidi kwa kutilia maanani kwamba, kiwango cha biashara na huduma kati ya Ufaransa na Algeria kimepungua sana na kufikia yuro bilioni moja na milioni 800 mwaka wa 2015. Wakati huo huo inatapasa kuelewa kuwa, Ufaransa na nchi za Umoja wa Ulaya kwa ujumla hazina hali nzuri ya kiuchumi na vilevile zinalazimika kuzidisha bajeti yao ya masuala ya kijeshi na kiusalama kutokana na kuongezeka hatari ya mashambulizi ya kigaidi barani humo.
Hata hivyo kwa kutilia maanani hitilafu za kisiasa zilizopo kati ya Ufaransa na Algeria, ni jambo lililo mbali kwa nchi hizo mbili kufikia maafikiano ya kuridhisha katika nyanja za kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kunyanyua juu kiwango cha biashara na huduma.
Kwa kutilia maanani historia ya uhusiano wa pande hizo mbili na hali ya sasa, inaonekana kuwa, ushirikiano wa nchi za kaskazini mwa Afrika na nchi za Magharibi hususan Ufaransa utaimarika na kufikia kiwango kinachohitajika baada ya nchi hizo kutupilia mbali malengo yao ya kikoloni, sera za kupenda kujitanua na siasa za kutaka kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.