Rais wa Misri alitaka jeshi kulinda usalama wa maeneo muhimu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i27544-rais_wa_misri_alitaka_jeshi_kulinda_usalama_wa_maeneo_muhimu
Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ametaka kuwekwa haraka vikosi vya ulinzi katika maeneo muhimu kwa ajili ya kulisaidia jeshi la polisi katika kulinda usalama wa miundombinu muhimu kwenye mikoa yote ya nchi hiyo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 10, 2017 02:38 UTC
  • Rais wa Misri alitaka jeshi kulinda usalama wa maeneo muhimu

Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ametaka kuwekwa haraka vikosi vya ulinzi katika maeneo muhimu kwa ajili ya kulisaidia jeshi la polisi katika kulinda usalama wa miundombinu muhimu kwenye mikoa yote ya nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya rais wa Misri imesema kuwa, Rais Abdel Fattah el-Sisi ametoa amri hiyo kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliyolenga makanisa mawili ya mji wa Tanta katikati ya mkoa wa al-Gharbiyah na Alexandria. El Sisi amelitaka jeshi kusimamia usalama wa maeneo muhimu ya nchi hiyo.

Katika hujuma za jana, karibu watu 50 waliuawa na zaidi ya wengine 100 kujeruhiwa. Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh limetangaza kuhusika na hujuma hiyo.

Baada ya mpripuko kutokea kanisani

Inafaa kuashiria kuwa, tangu ulipoondolewa madarakani utawala wa dikteta Hosni Mubarak, Misri imekuwa ikikumbwa na hali ya mchafukoge na mashambulizi ya kigaidi. 

Wakati huo huo Rais Abdel Fattah el-Sisi ametangaza hali ya hatari sambamba na kuunda baraza kuu la kupambana na ugaidi na kusimamia hali hiyo ya hatari nchini. Rais al-Sisi alitangaza hali hiyo muda mchache baada ya mashambulizi ya jana na kuongeza kuwa, kutokana na hali ya sasa nchini humo, anatangaza hali ya hatari kwa muda wa miezi mitatu. Kadhalika aliwataka Wamisri kushirikiana katika mapambano dhidi ya ugaidi na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuiunga mkono serikali yake katika vita hivyo.