17 wauawa katika mapigano kati ya magaidi na wanajeshi Mali
Askari wa Ufaransa wakishirikiana na wanajeshi wa Mali wamefanikiwa kuangamiza magaidi 12 kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiafrika.
Luteni Kanali Diarran Kone, Msemaji wa Jeshi la Mali amesema, magaidi hao wameangamizwa katika operesheni iliyopewa jina la Barkhane, iliyofaywa na wanajeshi wa Mali na Ufaransa, katika eneo la Gourma-Rharous, yapata kilomita 120 mashariki mwa mji wa Timbuktu.
Operesheni hii imejiri siku moja baada ya kundi hilo la kigaidi nchini humo kushambulia kambi ya jeshi ya Tagharost, lililoko umbali wa kilomita 150 kusini mwa mji wa Timbuktu.
Kundi la kigaidi la Nusrat al-Islam wal Muslimeen, lenye mafungamano na mtandao wa al-Qaeda tayari limetangaza kuhusika na hujuma hiyo dhidi ya kambi ya jeshi la Mali.
Wakati huohuo, askari wawili wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa na raia mmoja wamejeruhiwa baada ya gari lao kukanyaga guruneti, yapata kilomita 30 kusini mwa mji wa Tessalit, eneo la Kidal nchini Mali.
Haya yanajiri siku chache baada ya Herve Ladsous, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Operesheni za Kudumisha Amani za umoja huo kusema kuwa hali ya usalama nchini humo inatia wasiwasi, licha ya kutumwa wanajeshi wa UN na kupatikana mafanikio ya kiwango fulani katika kufikiwa makubaliano ya kusaka amani nchini humo.
Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa ambacho kilitumwa nchini Mali tangu Julai mwaka 2013, hadi sasa kimepoteza wanajeshi wake zaidi ya 70.