Apr 24, 2017 08:19 UTC
  • Makamu wa Rais wa Afrika Kusini ataka Rais Zuma achunguzwe

Makamu wa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema anaunga mkono kufanyika uchunguzi kuhusu madai ya ufisadi yanaoizunguka serikali ya Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo.

Ramaphosa amesema yuko tayari kushirikiana na Tume ya Kupambana na Ufisadi na asasi nyinginezo kuchunguza madai ya ufisadi dhidi ya serikali.

Mwezi Novemba mwaka jana, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Afrika Kusini aliitaka serikali iunde Kamisheni ya Mahakama ya kuchunguza madai hayo ndani ya siku 30, wito ambao Rais Zuma ameupuuza hadi leo. 

Wiki iliyopita, Ramaphosa alisema viongozi wanapaswa kuwasikiliza waandamanaji nchini humo ambao wanamtaka Rais Jacob Zuma ajiuzulu au aondolewe madarakani baada ya mabadiliko yake ya baraza la mawaziri kupelekea nchi hiyo kushushwa kiwango cha kiuchumi.

Rais Zuma

Kabla ya hapo, maelfu ya watu waliandamana huko Pretoria mji mkuu wa Afrika Kusini dhidi ya Rais Zuma wa nchi hiyo kufuatia mabadiliko aliyofanya katika baraza lake la mawaziri na kukabiliwa na ukosoaji mkubwa ndani.

Zuma anakabiliwa na mashinikizo hayo baada ya kumfuta kazi Pravin Gordhan, Waziri wa Fedha wa nchi hiyo aliyekuwa akiheshimiwa na matabaka mbalimbali nchini humo.

Mwaka jana, ripoti yenye kurasa 355 ilisema kuwa, ndugu wa familia moja  Ajay, Atul na Rajesh Gupta, wafanyabiashara wa Afrika Kusini wenye asili ya India walituhumiwa kuwa na mkono katika uteuzi wa mawaziri uliofanywa na Rais Zuma. 

Tags