Safari ya Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28402-safari_ya_papa_francis_kiongozi_wa_kanisa_katoliki_nchini_misri
Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Ijumaa ya jana alianza safari ya siku mbili nchini Misri. Safari ya Papa Francis nchini Misri inafanyika katika muendelezo wa stratejia ya mazungumzo na Uislamu wa wastani ambayo yalianza mwaka uliopita huko Roma kwa kuhudhuriwa na Ahmad Tayyib, Sheikh Mkuu wa al-Azhar.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Apr 29, 2017 03:19 UTC
  • Safari ya Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Misri

Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Ijumaa ya jana alianza safari ya siku mbili nchini Misri. Safari ya Papa Francis nchini Misri inafanyika katika muendelezo wa stratejia ya mazungumzo na Uislamu wa wastani ambayo yalianza mwaka uliopita huko Roma kwa kuhudhuriwa na Ahmad Tayyib, Sheikh Mkuu wa al-Azhar.

Mwaka uliopita Papa Francis alimkaribisha Sheikh Mkuu wa al-Azhar huko Vatican na kufanya naye mazungumzo na kwa muktadha huo akawa amehitimisha miaka mitano ya kutoaminiana baina ya Vatican na al-Azhar. Hali hiyo ya kutoaminiana baina ya pande mbili iliibuka baada ya Papa Benedict XVI kiongozi wa Kanisa Katoliki wakati huo kutoa matamshi dhidi ya Uislamu ambayo yalishadidisha mvutano baina ya pande hizo mbili.

Safari ya Papa Francis nchini Misri inatathminiwa kuwa na umuhimu hasa kwa kuzingatia mashambulio ya kigaidi ya hivi karibuni dhidi ya Wakristo wa Kibti. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaitazama safari ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani kama ina lengo la kuleta maridhiano baina ya Uislamu na Ukristo hasa kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni katika nchi hiyo. 

Rais wa Misri akimkaribisha Papa Francis

Kimsingi ni kuwa, kwa kuzingatiakwamba, Misri inakabiliwa na harakati kubwa ya matakfiri ukiwemo uwepo wa Daesh katika jangwa la Sinai na vile vile propaganda kubwa inayofanywa na magaidi hao ya kuwasajili vijana wa Kimsiri, ni miongoni mwa nchi inayohesabiwa kuwa inakabiliwa mno na tatizo la kuenea misimamo ya kuchupa mipaka. Nukta muhimu ni hii kwamba,  licha ya kuweko njama mtawalia za vyombo vya habari na baadhi ya viongozi wa madola ya Magharibi kama Donald Trump Rais wa Marekani za kutambua kwamba, Uislamu na vitendo vya kufurutu ada ni kitu kimoja, Papa Francis ametangaza bayana msimamo wake ambao ni kinyume na mtazamo huo. Katikati mwa Februari mwaka huu, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani alipinga madai ya kuweko kitu kinachojulikana kwa jina la ugaidi wa Kiislamu na akatangaza himaya yake kwa dini zote ulimwenguni.

Papa Francis alisisitiza kwamba, dini zinaeneza amani na kwamba, hatari ya uchupaji mipaka imo katika itikadi zote. Kwa mtazamo wa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani ni kuwa, hakuna kitu kinachoitwa ugaidi wa Kikristo kama ambavyo hakuna pia ugaidi wa Kiyahudi au ugaidi wa Kiislamu. Kwa hakika kujitokeza mashambulio ya kigaidi yanayofanywa na makundi yenye kuchupa mipaka hususan magaidi wa Daesh barani Ulaya na Marekani kumeandaa uwanja mwafaka wa kushadidishwa hujuma za kipropaganda na kuanzishwa vita vya kisaikolojia dhidi ya Uislamu na Waislamu. Propaganda hizi katika ulimwengu wa Magharibi hususan nchini Marekani ni kubwa zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine. Sababu ya hilo ni kuwa, Rais wa nchi hiyo Donald Trump ndiye kiongozi  wa propaganda na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo.

Sheikh Mkuu wa al-Azhar akiwa na Papa Francis

Wakati wa kampeni zake za uchaguzi wa Rais nchini Marekani, Trump akitumia kisingizio cha kupambana na ugaidi alitangaza kuwa, kuna ulazima wa Waislamu kuzuiwa kuingia katika ardhi ya Marekani. Matamshi hayo ya Trump yalikabiliwa na ukosoaji mkubwa ndani na nje ya nchi hiyo. Wakati huo huo, hatua zilizochukuliwa na Trump dhidi ya Waislamu baada ya kuingia katika ikulu ya Rais ya White House, zilishadidisha wasiwasi juu ya kuongezeka wimbi dhidi ya Uislamu na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu katika nchi za Magharibi. 

Misimamo hiyo ya kuchupa mipaka ya serikali mpya ya Marekani inaonyesha juu ya kuweko pengo kubwa si tu katika misimamo ya serikali ya sasa na iliyotangulia katika uwanja wa kutoa fasili na maana ya ugaidi na kutenganisha baina ya Uislamu na ugaidi, bali mtazamo huo wa Trump una upinzani mkubwa barani Ulaya ambapo kuna idadi kubwa ya Waislamu wanaoishi katika bara hilo.

Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani amekuwa akitaka kutofautishwa baina ya Uislamu na ugaidi. Merkel anasema kuwa, Uislamu katika dhati yake sio chimbuko la ugaidi na ni jambo la dharura kushirikishwa nchi za Kiislamu katika vita dhidi ya ugaidi. Wakati huo huo, inapaswa kubainishwa kwamba, kinyume na madai ya Magharibi ya chuki dhidi ya Uislamu ya kuwa kitu kimoja Uislamu, uchupaji mipaka na ugaidi ni idadi ndogo tu ya Waislamu ambao wana misimamo ya kufurutu ada huku akthari ya Waislamu wakipinga vikali vitendo vya utumiaji mabavu vinavyofanywa na kundi hilo dogo.

Kwa utaratibu huo, je ni sahihi kuvinasibisha na Uislamu na kuwahusisha Waislamu wote na vitendo vinavyofanywa na kundi dogo la Waislamu? Bila shaka si katika insafu na uadilifu kuinasibisha dini ya Uislamu na ugaidi, dini ambayo imesimama kwa misingi ya amani na huruma.