Kiongozi wa Ikhwanul Muslimin ya Misri ahukumiwa kifungo cha maisha jela
Mahakama ya Misiri imemhukumu kifungo cha maisha jela Mohamed Badie, kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo pamoja na wanachama wengine wawili wa harakati hiyo iliyopigwa marufuku.
Hukumu hiyo dhidi ya Badie na wenzake wawili imetolewa kwa madai ya kuhusika na machafuko yaliyotokea mwaka 2013 katika kulalamikia kuondolewa madarakani Muhammad Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo.
Maafisa wa mahakama pamoja na wakili wa utetezi Abdel Moneim Abdel Maksoud wameeleza kwamba mahakama ya Misri imemhukumu kifungo cha maisha jela kiongozi wa Ikhwanul Muslimin Mohamed Badie pamoja na Mahmoud Ghozlan, msemaji wa harakati hiyo na Hossam Abubakr, mjumbe wa Idara ya Miongozo.
Mnamo mwezi Aprili mwaka 2015, Badie pamoja na washtakiwa wengine 13 wanachama wa Ikhwanul Muslimin walihukumiwa kifo huku wanachama wengine 37 wa harakati hiyo ya Kiislamu ya Misri wakipewa adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa tuhuma za kile kilichotajwa kuwa ni kuunda "chumba cha operesheni" kwenye kambi ya waungaji mkono wa Morsi katika eneo la Rabaa Al-Adawiya, mjini Cairo mwaka 2013.
Mohamed Badie, ambaye anakabiliwa pia na mashtaka katika kesi nyengine 35 tayari alishahukumiwa kifo katika kesi nyengine tatu lakini hukumu hizo zilitenguliwa baadaye.
Harakati ya Ikhwanul Muslimin imekabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa vyombo vya dola tangu Morsi alipopinduliwa Julai 2013 katika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na mkuu wa majeshi wakati huo ambaye ni rais wa sasa wa nchi hiyo Abdel Fattah el-Sisi.
Watu zaidi 1,400 wameuliwa na wengine wasiopungua 22,000 wametiwa nguvuni huku mamia miongoni mwao wakihukumiwa kwa pamoja adhabu za vifo.../