Iran na Cameroon kuimarisha uhusiano wa pande mbili
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28892-iran_na_cameroon_kuimarisha_uhusiano_wa_pande_mbili
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Cameroon zimesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili hizi katika nyuga tofauti hususan ya kiuchumi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2017 03:05 UTC
  • Iran na Cameroon kuimarisha uhusiano wa pande mbili

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Cameroon zimesisitizia umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili hizi katika nyuga tofauti hususan ya kiuchumi.

Katika mkutano na Waziri wa Ulimwengu wa Kiislamu wa Cameroon mjini Yaounde hapo jana, Mahdi Aghajafari, Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuna fursa nyingi katika nyuga za uchumi, teknolojia na viwanda ambazo zinaweza kutumiwa na nchi mbili hizi kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Mbali na kuwasilisha barua ya Mohammad Javaz Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa mwenzake wa Cameroon akimualika hapa nchini, Aghajafari amesema kuna haja ya kuzishirikisha sekta za kibinafsi katika maendeleo na ushirkiano wa Tehran na Yaounde.

Waziri wa Ulimwengu wa Kiislamu wa Cameroon (Kulia) na maafisa wa Iran

Kwa upande wake, Edum Gregum, Waziri wa Ulimwengu wa Kiislamu wa Cameroon ameitaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuisaidia nchi hiyo ya Afrika kufanikisha miradi yake ya maendeleo.

Kadhalika pande mbili zimesisitizia haja ya kuimarisha ushirikiano wao katika masuala ya kieneo na kimataifa kama vile kupambana na ugaidi na misimamo ya kufurutu ada. Ieleweke kuwa, tangu mwaka 2014, Cameroon imekuwa ikikabiliwa  na msururu wa mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Aidha Iran na Cameroon zimekubaliana kuimarisha juhudi za kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu hususan kupitia Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.

Kabla ya kuitembelea Cameroon, Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alizitembelea nchi za Senegal, Nigeria na Ivory Coast.