May 13, 2017 02:34 UTC
  • Ukarabati wa msikiti mkubwa zaidi wa udongo wakamilika nchini Mali

Mamia ya wananchi Waislamu wa Mali wamekamilisha kazi ya matengenezo ya msikiti mkubwa zaidi wa matofali ya udongo duniani ulioko mjini Djenné kusini mwa nchi hiyo.

Kazi ya ukarabati iliyofanywa kwa ushirikiano wa mamia ya Waislamu wa Mali katika mji wa  Djenné ilikamilika siku ya Alkhamisi.

Kila mwaka wakaazi wa mji huo hukusanya na kuponda udongo kandokando ya Mto Bani na kushiriki kwa hamu na shauku kubwa katika shughuli ya ukarabati wa msikiti huo wa kihistoria.

Kwa kawaida shughuli ya kuufanyia matengenezo msikiti wa Djenné hufanyika katika siku maalumu ya mwaka inayojulikana kama "Sikukuu ya Udongo" ambayo hushirikisha matabaka tofauti ya jamii ya Waislamu nchini Mali.

Waislamu wa Mali wakiufanyia ukarabati msikiti wa Djenne

Ujenzi wa msikiti wa Djenné ulianza mwaka 1906 na kukamilika mwaka 1907, ambapo mwaka 1988 msikiti huo pamoja na miji ya kale ya Djenné vilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuwa moja ya maeneo ya Turathi za Dunia.

Zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Mali ni Waislamu; na katika kila mji na kijiji nchini humo kuna vyuo na madrasa za kusomesha Quráni kwa ajili ya watoto wadogo.../

Tags