9 wauawa katika mapigano kaskazini mwa Misri
Watu tisa wameuawa katika mapigano yaliyotokea jana kwenye Rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri.
Mapigano hayo yamezuka baina ya wanajeshi na watu wenye silaha kusini mwa mji wa Rafah katika Rasi ya Sinai. Watu saba wenye silaha wameuawa kwenye mapigano hayo.
Wakati huo huo afisa mmoja wa Misri ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa, raia wawili wametekwa nyara na baadaye kuuawa katika miji ya Rafah na al Arish katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri.
Rasi ya Sinai ni eneo linaloshuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya kigaidi. Mashambulizi hayo yameongezeka tangu mwezi Novemba 2014 baada ya kundi moja la kigaidi katika eneo hilo kutangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la Daesh yaani ISIS.
Mashambulizi mengi ya kigaidi ya miaka ya hivi karibuni yamekuwa yakifanywa na kundi la Ansar Bait al Muqaddas lililotangaza utiifu wake kwa genge la kigaidi la Daesh.
Baada ya kutangaza utiifu wake kwa magaidi wa ISIS, kundi hilo limebadilisha jina na kujiita Wilaya ya Sinai.